HRW yatahadharisha kuhusu njama mpya za Israel katika Quds Tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33076-hrw_yatahadharisha_kuhusu_njama_mpya_za_israel_katika_quds_tukufu
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetahadharisha kuhusu mipango na njama za muda mrefu zinazotekelezwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa madhumuni ya kuwahamisha wakaazi wote Wapalestina wa asili katika mji wa Baitul Muqaddas na kuuzayunisha mji huo.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Aug 13, 2017 03:41 UTC
  • HRW yatahadharisha kuhusu njama mpya za Israel katika Quds Tukufu

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) limetahadharisha kuhusu mipango na njama za muda mrefu zinazotekelezwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwa madhumuni ya kuwahamisha wakaazi wote Wapalestina wa asili katika mji wa Baitul Muqaddas na kuuzayunisha mji huo.

Kwa mujibu wa HRW, hatua ya kubatilisha vibali vya kuishi vya maelfu ya Wapalestina katka mji wa Quds mbali na kuwa ni sera inayofuata vigezo vya kindumakuwili lakini pia imeweka masharti yasiyotekelezeka ya ukaazi kwa wakaazi wa mji huo mtakatifu.

Ripoti iliyotolewa na shirika hilo la kimataifa la haki binadamu inaeleza kuwa tangu mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) ulipovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1967 hadi mwaka uliopita wa 2016, Israel imebatilisha vibali visivyopungua 14,595 vya ukaazi vya Wapalestina wanaoishi Baitul Muqaddas Mashariki na kuwalazimisha wauhame mji wao huo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Human Rights Watch, uvamizi huo hatari uliofanywa na utawala wa Kizayuni unapingana na sheria za kimataifa, na hadi ifikapo mwaka 2020 mpango huo utakuwa umepunguza idadi ya Wapalestina wanaoishi katika mji wa Quds kwa asilimia 12.

Mandhari ya mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu

Wakati huohuo Dakta Hanna Issa, Katibu wa Kamati ya Kiislamu na Kikristo ya Kuihami Quds na Maeneo Matakatifu ametangaza kuwa Israel haitosheki na kuwafukuza Wapalestina, bali inaendeleza sera ya kuzuia watoto wanaozaliwa wasisajiliwe utambulisho wao kwenye hati za utambulisho za wazazi wao, hatua ambayo inalenga kuizayunisha Quds na kuhakikisha hakuna Mpalestina yeyote anayesalia ndani ya mji huo.

Hanna Issa

Katibu wa Kamati ya Kiislamu na Kikristo ya Kuihami Quds na MaeneoMatakatifu amebainisha kuwa tangu mwaka 1967 hadi mwaka 1993 kuna Wapalestina zaidi ya 1,40,000 waliofukuzwa katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan kwa sababu ya hati za utambulisho na wengine 18,887 wamehamishwa katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Hanna Issa ameongeza kuwa hivi sasa kuna familia zaidi ya 200 za Wapalestina ambazo zimeshapewa barua za onyo la kubomolewa nyumba zao na mamlaka za utawala wa Kizayuni na kusisitiza kuwa kuwaunga mkono kimaanawi tu wakaazi wa Baitul Muqaddas hakutoshi bali Wapalestina hao wanahitaji pia misaada ya kimaada na kifedha kwa ajili ya kugharamia huduma za afya, elimu na maskani.../