Hizbullah: Magaidi wa Daesh (ISIS) hawakuwa na budi ila kujisalimisha
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema wanachama waliokuwa wamejizatiti kwa silaha wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika eneo la Qalamun, hawakuwa na chaguo jingine ghairi ya kujisalimisha kwa vikosi vya muqawama baada ya vikosi hivyo kuwakaribia magaidi hao katika eneo la mpaka wa pamoja wa Lebanon na Syria.
Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo jana Jumatatu alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu kuhamishiwa magaidi hao kwenye eneo la Deir ez-Zor, mashariki mwa Syria na kuongeza kuwa, wanachama hao wa genge la ukufurishaji wa Daesh waliishiwa na maarifa na mbinu za makabiliano na hivyo wakalazimika kunyanyua mikono juu baada ya kujikuta kwenye mzingiro wa wanaharakati wa muqawama.
Sambamba na kuwapongeza wanamuqawama na wanajeshi wa Lebanon kwa ushindi huo, Sayyid Nasrullah amebainisha kuwa, ugaidi ni harakati za kitakfiri na katika wimbi la njama za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kushinikiza sera zao za kibeberu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Baadhi ya duru zimeripoti kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeipatia harakati ya Hizbullah taarifa kuhusu askari wa jeshi la Lebanon waliotekwa nyara na kundi hilo. Vikosi vya muqawama vitakabidhiwa viwiliwili vya mashahidi wanne waliozikwa kwenye eneo la Wadi Mira, huko Qalamun nchini Syria.
Tarehe 19 ya mwezi huu wa Agosti, jeshi la Lebanon lilianzisha operesheni iliyopewa jina la Fajrul-Jurud dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, iliyokuwa na lengo la kuwafurusha matakfiri hao kutoka eneo la Qalamun, yapata kilomita 330 kaskazini mwa mji mkuu wa Syria, Damascus.
Katibu Mkuu wa harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon amesema operesheni hiyo imefanikiwa na imefikia malengo yake yoye iliyoyakusudia.