HRW yakosoa wimbi jipya la kamata kamata dhidi ya wapinzani Saudia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa vikali wimbi jipya la kamata kamata inayofanywa na maafisa usalama wa Saudi Arabia dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake wakiwemo wanazuoni.
Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo katika eneo la Mashariki ya Kati amesema kamata kamata, kuzuiliwa na kupandishwa kizimbani kinyume cha sheria kunakofanywa na utawala wa Riyadh dhidi ya wanaharakati wapenda amani wa nchi hiyo ni ithibati tosha kuwa Saudi Arabia imeshindwa kuwavumilia raia wake wanaopigania haki za binadamu na mageuzi kwa njia za amani.
Amesema ni jambo la kusikitisha namna Saudia inaendelea kuwazuilia wanaharakati hao kwa misingi ya siasa nyuma ya pazia la kupambana na ugaidi.
Miongoni mwa shakhsia na wanazuoni zaidi ya 20 wa Kiislamu waliokamatwa na maafisa usalama wa Aal-Saud hivi karibuni ni Salman al-Awudah na Iwadh al-Qarani, ambao hivi karibuni walikosoa misimamo hasi ya Riyadh na washirika wake yaani Misri, Imarat na Bahrain, dhidi ya Qatar.
Tayari Jumuiya ya Kimataifa ya Wanazuoni wa Kiislamu (IUMS) imeutaka utawala wa kifalme wa Aal-Saud uwaachie huru makumi ya wahubiri na wasomi hao wa Kiislamu uliowakamata hivi karibuni.