Iraq kuwahukumu wanachama wa ISIS, raia wa Ulaya
Vyombo vya mahakama nchini Iraq vinatazamiwa kuwatolea hukumu ikiwemo hukumu ya kifo, makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) raia wa nchi za Ulaya.
Jawad al-Chlaihawi, balozi wa Iraq nchini Ubelgiji amenukuliwa na kanali ya televisheni ya RTBF akisema kuwa, wanachama wa Daesh wapatao 100 raia wa nchi za Ujerumani, Ufaransa, Russia na Ubelgiji wamekamatwa na vyombo vya usalama vya Iraq na wanasubiri hukumu dhidi yao.
Duru za habari zinaarifu kuwa, baadhi ya wanachama hao wa Daesh ni raia wa nchi za Chechnya, Uturuki na nchi za Asia ya Kati.
Kanali Ahmed al-Taie, kamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Iraq ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya Kiarabu vinawashikilia pia mamia ya familia za wanachama wa ISIS wakisubiri maagizo kutoka serikali ya Baghdad.
Watu wenye misimamo ya kufurutu ada kutoka nchi za Ulaya walianza kujiunga na kundi la Daesh kwa umati mwaka 2014, baada ya genge hilo la kitakfiri kuanzisha harakati za umwagaji damu na uharabifu katika nchi za Iraq na Syria.
Kwa mujibu wa serikali ya Ufaransa, raia 700 wa nchi hiyo ya Ulaya, wakiwemo watoto 500 wanaishi katika ngome zinazodhibitiwa na Daesh huko Iraq na Syria.