Marekani yakiri, Jabhatu Nusra imetumia silaha za kemikali nchini Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i35837-marekani_yakiri_jabhatu_nusra_imetumia_silaha_za_kemikali_nchini_syria
Wizara ya Ulinzi ya Russia leo tarehe 20 Oktoba imetangaza kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa Marekani imekiri kuwa kundi la kigaidi la Jabhatu Nusra limetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Syria.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Oct 20, 2017 22:56 UTC
  • Marekani yakiri, Jabhatu Nusra imetumia silaha za kemikali nchini Syria

Wizara ya Ulinzi ya Russia leo tarehe 20 Oktoba imetangaza kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa Marekani imekiri kuwa kundi la kigaidi la Jabhatu Nusra limetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Syria.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Russia, Meja Jenerali Igor Konashenkov amesema mbali na kukiri ukweli huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pia imesisitiza kuwa magaidi wa kundi la Jabhatu Nusra wametumia silaha za kemikali katika mashambulizi yao ya kigaidi nchini Syria.

Makumi ya watu waliuawa katika mashambulizi ya silaha za kemikali Khan Sheikhun, Syria.

Maudhui ya utumiaji wa silaha za kemikali imekuwa miongoni mwa mambo yaliyozusha mjadala na makelele mengi katika mgogoro wa sasa wa Syria. Wapinzani wa serikali ya Damascus wakishirikiana na nchi kama Marekani na Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel zinadai kuwa serikali ya Syria ndiyo iliyotumia silaha za kemikali dhidi ya raia katika maeneo kama Ghouta Mashariki na Khan Sheikhun. Hata hivyo kambi hiyo imeshindwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai hao ambayo yamekuwa yakipingwa vikali na serikali ya Syria. Si hayo tu bali mwaka 2013 serikali ya Syria iliafiki kuondolewa silaha zote za kemikali nchini humo na kupelekwa nje kwa shabaha ya kondoa visingizio vyote vinavyotumiwa na wapinzani hususan Marekani. 

Jabhatu Nusra ambayo ni tawi la kundi la kigaidi la al Qaida, liliamua kubadili jina na kujiita Jabhatu Fat'hi Sham kwa shabaha ya kujitofautisha na makundi mengine ya kigaidi yanayopigana na serikali ya Syria. Kundi hili ambalo sasa Marekani imekiri kuwa lilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia, limekuwa likitambuliwa na serikali ya Washington kuwa ni miongoni mwa makundi ya upinzani nchini Syria yenye misimamo eti ya wastani. Marekani ililitea kundi hilo na kuliunga mkono licha ya vyombo mbalimbali wakiwemo maafisa wa jumuiya za Umoja wa Ulaya kusisitiza kwamba, limetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Syria.

Magaidi wa Jabhatu Nusra, Syria

Katika mkondo huo Katibu Mkuu wa Shirika la Usalama na Habari la Ulaya Balozi Haitham Abu Saeed mwezi Mei mwaka jana alisema kuwa, kundi la Jabhatu Nusra linatumia silaha za kemikali linazopokea kutoka kwa Saudi Arabia. Haitham Abu Saeed aliongea kuwa: Silaha hizo zinavushwa kutoka Bulgaria na kuwasilishwa kwa magaidi nchini Syria kupitia kwenye mipaka ya Jordan".

Kwa msingi huo inaeleweka wazi kwamba, silaha hizo za kemikali zinazotumiwa kuua raia wasio na hatia nchini Syria zinafikishwa kwa makundi ya kigaidi na nchi kama Saudi Arabia na Marekani ambazo ndizo zilizo mstari wa mbele kuituhumu Damascus kuwa imetumia silaha za kemikali dhidi ya raia! Hii ina maana kwamba, nchi hizo yaani Marekani, Saudi Arabia na washirika wao, badala ya kukiri kwamba zimekuwa zikiyasaidia makundi ya kigaidi huko Syria kwa aina mbalimbali ya silaha zikiwemo za kemikali, zinaituhumu serikali ya Damascus kuwa ndiyo iliyotumia silaha hizo kwa shabaha ya kuchochea walimwengu dhidi ya serikali ya Rais Bashar Asad wa Syria na kuidhihirisha kuwa ni utawala wa kikatili. 

Magaidi wa Jabhatu Nusra wamekuwa wakiungwa mkono na Marekani

Pamoja na hayo na licha ya Marekani kukiri kwamba kundi la Jabhatu Nusra limetumia silaha za kemikali dhidi ya raia wa Syria, lakini bado inashinikiza suala la kurefusha muda wa majukumu ya kamati ya Umoja wa Mataifa na Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali nchini humo. Inatazamiwa kuwa ripoti ya pamoja na taasisi hizo mbili kuhusu mashambulizi ya silaha za kemikali yaliyofanyika katika eneo la Khan Sheikhun itatangazwa tarehe 26 mwezi huu wa Oktoba.