Polisi 12 wauawa na kujeruhiwa nchini Misri
Duru za usalama za Misri zimetangaza habari ya kushambuliwa gari la polisi wa nchi hiyo na watu wenye silaha katika mkoa wa Sinai Kaskazini.
Duru hizo zimetangaza kuwa, watu wenye silaha wameripua bomu la kutegwa pembeni mwa barabara lililokuwa linaongozwa kwa mbali katika viungwa vya al Arish, makao makuu ya mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri na baadaye kuanza kuwashambulia kwa risasi maafisa wa polisi waliokuwemo kwenye gari hilo.
Duru hizo za usalama za Misri zimeongeza kuwa, maafisa wawili wa polisi wameuawa na wengine 10 wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo la kushtukiza.
Mkoa wa Sinai Kaskazini ulioko kwenye ukanda wa kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika umekuwa ni maficho ya makundi mbalimbali ya kigaidi likiwemo lile la Answar Bayt al Muqaddas ambalo mwezi Novemba 2014 lilitangaza rasmi kujiunga na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) na baadaye kujibadilisha jina na kujiita Wilaya ya Sinai.
Katikati ya mwezi huu wa Oktoba, jeshi la Misri lilitangaza habari ya kuua wanachama 24 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) katika Peninsula ya Sinai.
Taarifa ya jeshi hilo ilisema kuwa, magaidi hao wakufurishaji walishambuliwa na kuangamizwa baada ya kujaribu kuvamia kituo cha kijeshi kusini mwa mji wa Sheikh Zuweid, kwa mabomu ya kutegwa garini na maguruneti.