Wazayuni waunda kikosi kipya cha polisi ili kuwakandamiza zaidi Waislamu
Waziri wa usalama wa ndani wa utawala wa Kizayuni wa Israel ametoa amri ya kuundwa kikosi kingine maalumu kitakachowakandamiza Wapalestina katika Msikiti wa al Aqsa.
Habari hiyo imetangazwa na Kanali ya Pili ya televisheni ya utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa, kikosi hicho kipya cha jeshi la polisi la Israel kitatumia teknoloja za kisasa wakiwemo askari 100 waliopata mafunzo maalumu ya kuwakandamiza Waislamu wa Palestina.
Ingawa televisheni hiyo ya Kizayuni imedai kuwa kazi ya kikosi hicho maalumu itakuwa ni kulinda usalama na utulivu wa watu wote ndani ya Msikiti wa al Aqsa lakini kila mtu anatambua kuwa lengo la kikosi hicho litakuwa ni kuwakandamiza zaidi Waislamu na kuwazuia kutekeleza ibada katika Kibla cha Kwanza cha Waislamu duniani.
Utawala wa Kizayuni umedai kwamba lengo la kikosi hicho litakuwa ni kulinda usalama wa wote katika hali ambayo, Israel imeligeuza eneo hilo takatifu kuwa sehemu ya kuonesha jeuri na ujuba wa walowezi wa Kizayuni na shabaha yake kuu ni kufuta utambulisho wa Kiislamu na Kikristo wa eneo hilo na badala yake kuligeuza kuwa eneo la Kizayuni.
Kila siku wimbi kubwa la walowezi wa Kizayuni wanaingia ndani ya Msikiti wa al Aqsa kwa ulinzi na msaada kamili wa wanajeshi ghasibu wa Israel. Uvamizi huo wa walowezi wa Kizayuni umekuwa ukizusha Intifadha za mara kwa mara za Wapalestina wanaopambana na ukatili wa Wazayuni hao.