Marekani kuipa Israel dola milioni 705 kujiimarisha kwa makombora
Katika hali ambayo Marekani imezusha kelele nyingi kuhusu miradi ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mabaraza ya Congress na Senate ya nchi hiyo yamefikia mwafaka wa kuupatia utawala wa Kizayuni wa Israel msaada wa dola milioni 705 kwa ajili ya kuendeleza miradi yake ya makombora.
Shirika la habari la FARS lilitangaza jana kwamba, bajeti iliyotengwa na baraza la Congress la Marekani kama sehemu ya msaada wa kila mwaka wa kuendeleza mfumo wa makombora wa Israel umekuwa ni zaidi ya dola miloni 558 kutokana na ombi la serikali ya rais wa nchi hiyo Donald Trump.
Mwaka jana na katika kipindi cha mwishoni mwa serikali ya Barack Obama, Marekani ilitiliana saini na utawala wa Kizayuni wa Israel mkataba wa miaka 10 wa kiulinzi wenye thamani ya dola bilioni 38.
Misaada hiyo mikubwa isiyo na masharti inatolewa na Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika hali ambayo kila leo utawala huo ghasibu unaendelea kuua kinyama watu wasio na hatia huko Palestina.
Kichekesho kikubwa zaidi ni kwamba, Marekani inauimarisha utawala wa Kizayuuni kwa silaha za kisasa kabisa ikiwa ni pamoja na kutenga mamilioni ya dola kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa makombora wa utawala huo katili katika hali ambayo hiyo hiyo Marekani imezusha makelele mengi duniani kupinga haki ya Iran ya kuimarisha mfumo wake wa makombora ambao ni wa kujilinda na kujihami tu na mashambulizi ya adui.