Hamas: Mossad ndiyo iliyomuua kigaidi Muhammad al Zawawi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36438-hamas_mossad_ndiyo_iliyomuua_kigaidi_muhammad_al_zawawi
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa shirika la ujasusi la Israel, Mossad ndilo lililohusika na mauaji ya kigaidi ya mtaalamu wa masuala ya anga wa Tunisia ambaye pia alikuwa mtaalamu wa kutengeneza ndege zisizo na rubani wa harakati hiyo, Muhammad al Zawawi.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Nov 16, 2017 12:19 UTC
  • Hamas: Mossad ndiyo iliyomuua kigaidi Muhammad al Zawawi

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa shirika la ujasusi la Israel, Mossad ndilo lililohusika na mauaji ya kigaidi ya mtaalamu wa masuala ya anga wa Tunisia ambaye pia alikuwa mtaalamu wa kutengeneza ndege zisizo na rubani wa harakati hiyo, Muhammad al Zawawi.

Mjumbe wa ngazi ya juu wa Hamas, Muhammad Nizal amesema kuwa, matokeo ya uchunguzi kuhusu mauaji ya kigaidi la Muhandisi Muhammad al Zawawi yanaonesha kuwa Mossad ndiyo iliyohusika na mauaji hayo kwa msaada wa kilojestiki wa pande nyingine kadhaa.

Muhammad Nizzal ameongeza kuwa, operesheni ya mauaji ya kigaidi dhidi ya al Zawawi ilipangwa mwaka mmoja kabla ya kufanyika kwake na kwamba wahalifu waliofanya mauaji hayo waliingia Tunisia kwa kutumia pasi za kusafiria za Bosnia. 

Mjumbe huyo wa ngazi ya juu wa Hamas amesisitiza kuwa hilo halikuwa shambulizi la kwanza la kigaidi kufanywa na Israel dhidi ya wanapambano wa Paletina katika ardhi ya Tunisia na kwamba shirika la ujasusi la Mossad linapaswa kuandamwa kutokana na jinai hizo. 

Muhammad al Zawawi

Muhandisi Muhammad al Zawawi ambaye alikuwa mwanachama wa Batalioni ya Izzuddin Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas aliuawa kigaidi tarehe 15 Disemba mwaka 2015 mbele ya nyumba yake katika mkoa wa Sfax nchini Tunisia. 

Hivi karibuni mkuu wa shirika la ujasusi la Israel, Mossad, Yossi Cohen alikiri kwamba kila mwaka utawala huo ghasibu unatekeleza maelfu ya operesheni na kwamba baadhi yazo huwa ngumu sana katika nchi za kigeni.