Mufti Mkuu wa Russia ataka kupelekwa misaada ya kibinadamu Syria
Mufti Mkuu wa Russia amezitolea wito nchi za Kiarabu zitume misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Syria.
Sheikh Tala'at Tajuddin jana alisema kuwa wafuasi wote wa dini za Mwenyezi Mungu wanapasa kushiriki katika kuandaa shehena za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Syria. Mufti Mkuu wa Russia ameashiria pia kutumwa shehena ya misaada ya kibinadamu kutoka vituo vya kidini vya nchi hiyo kwa ajili ya wananchi wa Syria.
Akizungumza juzi Jumamosi katika kikao na viongozi wa Kanisa la Orthodox la nchini Russia, Rais Vladimir Putin wa Russia alilitolea wito kwa kanisa hilo lishiriki katika kuijenga upya Syria na kutumia nafasi iliyonayo kimataifa kufanikisha lengo hilo. Vita vinavyoendeshwa na magaidi na waungaji mkono wao dhidi ya wananchi na serikali halali ya Syria hadi sasa vimesababisha vifo na kujeruhi mamia ya maelfu ya Wasyria na kuwafanya wengine zaidi ya milioni 12 kuwa wakimbizi.
Vita hivyo pia vimeharibu miundo mbimu katika aghalabu ya maeneo ya nchi hiyo. Benki ya Kimataifa ya Ujenzi Mpya na Ustawi yenye mfungamano na Benki ya Dunia imetangaza kuwa pato la taifa la thamani ya dola bilioni 226 limeaathiriwa katika vita vilivyoanza huko Syria kuanzia mwaka 2011 hadi mwishoni mwa mwaka jana wa 2016.