UN: Kombora lililovurumishwa Riyadh Saudi Arabia si la Iran
Naibu msemaji wa Umoja wa Mataifa usiku wa kuamkia leo amesisitiza kuwa, hakuna ushahidi wowote unaoweza kuthibitisha madai kwamba makombora yanayotumiwa na jeshi la Yemen kuipiga Saudi Arabia yanatoka nchini Iran.
Farhan Haq aidha amesema, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kila baada ya miezi sita huwa anatoa ripoti kuhusiana na utekelezaji wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la umoja huo na kwamba katika ripoti hiyo iliyofanyiwa utafiti na uchunguzi wa kina kuna sehemu inazungumzia pia makombora yanayovurumishwa nchini Saudi Arabia kutokea Yemen, lakini hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha kuwa makombora hayo yanatengenezwa nchini Iran. Ripoti hiyo iliwasilishwa jana Alkhamisi kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Usiku wa kuamkia leo, mwakilishi wa kudumu wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amedai kuwa, mabaki ya makombora ya Iran yamepatikana katika ardhi ya Saudia, madai yasiyo na msingi ambayo yamepingwa haraka sana na hata na Umoja wa Mataifa.
Baada ya kuona wameshindwa katika njama zao dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen, wavamizi wa nchi hiyo maskini ya Kiarabu wakiongozwa na Saudi Arabia, sasa wanadai kuwa eti Iran inalipa jeshi la Yemen silaha za kukabiliana na wavamizi hao kama njia ya kuhalalisha kufeli kwao vibaya katika uvamizi wao huo.
Mara kwa mara viongozi wa Yemen wamekuwa wakikanusha madai hayo na kusema kuwa, makombora yanayotumiwa na jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi yanatengenezwa ndani ya Yemen hasa kwa kuzingatia kuwa Saudi Arabia imeizingira kila upande nchi hiyo, kutokea angani, majini na ardhini.