Qatar yaishitaki Imarati UNSC kutokana na hatua zake za kichokozi
(last modified Fri, 12 Jan 2018 04:19:56 GMT )
Jan 12, 2018 04:19 UTC
  • Qatar yaishitaki Imarati UNSC kutokana na hatua zake za kichokozi

Mwakilishi wa Qatar katika Umoja wa Mataifa amewasilisha mashitaka kwa Baraza la Usalama la Umoja dhidi ya Imarati kutokana na hatua yake ya kichokozi ya kukiuka anga yake.

Katika barua aliyoiwasilisha kwa Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Alya bint Ahmed Al Thani, amesema kuwa tarehe 21 Disemba mwaka jana, ndege moja ya kivita ya Imarati iliruka katika urefu wa futi elfu 33 katika anga la eneo la kiuchumi la Qatar. Kadhalika barua hiyo imesisitiza kwamba, hatua hiyo ya Imarati ni kinyume kabisa cha sheria za kimataifa za haki ya kujitawala nchi husika.

Ndege ya kivita ya Imarati ikiwa katika anga ya Qatar

Mwakilishi wa kudumu wa Qatar katika Umoja wa Mataifa Alya bint Ahmed Al Thani, amekitaja kitendo hicho kuwa cha uchochezi na cha uadui na amefafanua kuwa, serikali ya Doha imejiandaa kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kulinda mipaka, anga yake na usalama wa taifa.

Itakumbukwa kuwa, katika miezi ya hivi karibuni Saudi Arabia, Imarati, Misri na Bahrain zilichukua hatua mbalimbali za uhasama dhidi ya Qatar kwa lengo la kuishinikiza serikali ya Doha kutii matakwa yao. Katika uwanja huo, Riyadh na waitifaki wake kuanzia tarehe tano Juni 2017 zilikata mahusiano yote ya kidiplomasia na Qatar sambamba na kuizingira nchi hiyo katika pande zote za ardhini, angani na baharini.

Bendera za nchi zilizoiwekea mzingiro Qatar

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alisema kuwa, lau ingelitaka, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingeliweza kutumia tofauti za kisiasa zilizopo kati yake na Doha kuwatesa kwa njaa wananchi wa Qatar baada ya nchi hizo nne za Kiarabu kuizingira nchi hiyo, lakini kamwe haikufanya hivyo.

Tags