Feb 06, 2018 08:00 UTC
  • Juhudi za Marekani za kuvuruga usalama wa Syria

Mwandishi na mtaalamu mmoja wa masuala ya kisasa wa nchini Marekani amesema kuwa nchi hiyo inafanya juhudi kubwa za kuuhadaa ulimwengu kuhusiana na suala la Syria.

Akizungumza hivi karibuni na kanali ya habari ya PressTV, Adam Gray amesema kila mara jeshi la Syria na wapiganaji wa muhimili wa mapambano ya Kiislamu wanapopata mafanikio na ushindi dhidi ya magaidi, Marekani huibua madai yasiyo na msingi eti Syria inatumia silaha za kemikali dhidi ya raia wake ili kuhadaa na kuipotosha jamii ya kimatafa kwa shabaha ya kuusaidia utawala ghasibu wa Israel uendeleze siasa zake za kukalia kwa mabavu ardhi za Waislamu na Waarabu. Huku akiashiria kushindwa Marekani katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika jana Jumatatu kuhusu Syria, Adam Gray amesema kuwa Marekani inafanya juhudi kubwa kutumia vibaya suala la silaha za kemikali kama chombo cha kutoa mashinikizo na kueneza propaganda chafu dhidi ya Syria na Russia.

Askari wa Marekani wakiwa katika ardhi ya Syria kinyume cha sheria za kimataifa

Gray pia amekosoa matamshi ya Nikki Haley, mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa kuhusu madai ya kuwepo silaha za kemikali nchini Syria na kusisitiza kuwa katika hali ya hivi sasa Syria haina silaha hizo, jambo ambalo ilimwengu mzima unalijua vizuri na kwamba njama hizo za Marekani dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu zitafeli tu. Nchi za Magharibi na hasa Marekani zinatoa madai yasiyo na msingi kuwa serikali ya Syria inatumia sialaha za kemikali dhidi ya raia wake ili kuhadaa fikra za waliowengi na kupotosha ukweli wa mambo, kwa madhumuni ya kujaribu kufunika ushindi mkubwa lilioupata jeshi la Syria pamoja na wapiganaji wa mrengo wa mapambano ya Kiislamu dhidi ya magaidi.

Tags