Apr 16, 2018 04:18 UTC
  • Mfalme wa Saudia akariri madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran

Mfalme wa Saudi Arabia kwa mara nyingine amekariri madai yasiyo na msingi na kudai kuwa eti Iran inaingilia mambo ya ndani ya Yemen na kuwa inaunga mkono ugaidi.

Mfalme Salman bin Abdul Aziz Aal Saudi alitoa matamshi hayo yasiyo na msingi siku ya Jumapili katika mkutano wa 29 wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya  ya Nchi za Kiarabu mjini Dhahran. Mtawala huyo wa Saudia ameituhumu Iran kuwa eti inawaunga mkono wapiganaji Wahouthi nchini Yemen na kwamba imewatumia makombora ya balistiki. Mfalme wa Saudia aidha amekariri madai yake yaliyojaa uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuituhumu kuwa eti inaunga mkono ugaidi na kuchangia ukosefu wa uthabiti katika eneo.

Madai hayo yasiyo na msingi dhidi ya Iran yanatolewa na utawala wa Saudia ambao kwa kushirikiana na Imarati, umekuwa ukiwaua watu wa Yemen tokea mwaka 2015 kwa silaha za Marekani na Uingereza.

Watoto ni waathirika wakuu wa jinai za Saudia nchini Yemen

Wasaudia wanajaribu kufunika kushindwa kwao nchini Yemen na sasa wameshindwa kukabiliana na uhalisia wa mambo katika eneo. Wasaudia kabla ya kutoa tuhuma zozote wanapaswa kujibu kuhusu jinai zao dhidi ya Yemen, ambapo wameua zaidi ya watu 14,000 hadi sasa, wengi wakiwa ni wanawake na watoto mbali na kuwajeruhi wengine wengi huku mamilioni wakibakia bila makao na wakikumbwa na baa la njaa.

Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitilia mkazo uhusiano mwema na nchi jirani kama kipaumbele cha sera zake za kigeni sambamba na kujaribu kutatua matatizo ya eneo kupitia mazungumzo ili kudumisha uthabiti na usalama wa mataifa ya eneo hili.

Tags