Apr 20, 2018 13:53 UTC
  • Kufichuliwa uhusiano mkubwa uliopo baina ya Saudia na Israel

Gazeti la al Manar la Palestina limechapisha ripoti inayosema kuwa, mfalme wa Saudi Arabia ndiye muhandisi wa uhusiano wa Wasaudia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuandika kuwa: Tangu mwanzoni mwa mwaka 1990, mfalme wa hivi sasa wa Saudia ana uhusiano wa karibu na Israel.

Gazeti hilo la Palestina limezinukuu duru za kuaminika zikifichua kuwa: Mawasiliano ya siri na ya kificho baina ya Salman bin Abdulaziz Aal Saud, mfalme wa hivi sasa wa Saudi Arabia na Israel yamekuwepo tangu Salman alipokuwa amir wa Riyadh. Tangu wakati huo alikuwa na mawasiliano ya karibu na watu kama Is'haq Rabin, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Ripoti ya gazeti hilo imesisitiza kuwa, Salman alimuunganisha mwanawe Muhammad bin Salman kwenye mawasiliano hayo maalumu na Israel tangu miaka kadhaa nyuma.

Jinai za Waisrael dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina hazina kikomo. Lakini viongozi wa Saudia wanasema Israel ina haki

 

Hivyo si jambo la kushangaza kumsikia Muhammad bin Salman akiliambia jarida moja la Marekani la The Atlantic hivi karibuni kwamba Riyadh ina manufaa mengi ya pamoja na Israel na kwamba Waisraeli wana haki ya kuwa na ardhi yao, ikiwa ni kutangaza hadharani na mbele ya walimwengu kuwa anaunga mkono jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.

Ripoti ya gazeti la al Manar la Palestina imesambazwa katika hali ambayo, mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz alisema hivi karibuni katika kikao cha 29 cha viongozi wa nchi wanachama wa umoja wa nchi za Kiarabu kwamba eti hicho ni kikao cha Quds ili kwa njia hiyo aweze kuwafumba macho walimwengu na kuonesha kuwa anaumizwa na dhulma wanayofanyiwa Wapalestina.

Misimamo hiyo ya nyuso mbili na ya kukinzana ya ukoo wa Aal Saud ni uthibitisho wa wazi wa kilele cha ulaghai na njama zao za kujaribu kuficha kashfa na jinai kubwa wanazozifanya katika mataifa kadhaa ya Kiarabu hasa huko Yemen, Iraq na Syria.

Waisrael wanawapiga mabomu ya sumu na ya kemikali wananchi wa Palestina lakini dunia imekaa kimya huku Marekani, Ufaransa na Uingereza zikiishambulia Syria kwa madai ya uongo ya mashambuli ya kemikali

 

Gazeti la al Sharq la nchini Qatar nalo limechapisha ripoti na kufichua tena waraka unaoonesha kuwa, kabla ya vita vya mwaka 1967 baina ya Waarabu na Israel, Riyadh iliichochea Marekani kuiunga mkono Israel katika mashambulizi yake dhidi ya Misri na Syria na kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina. Gazeti hilo la nchini Qatar limeandika: Matamshi ya Muhammad bin Salman alipohojiwa na jarida la Marekani la The Atlantic ya kwamba Waisraeli wana haki za kuwa na ardhi yao, si jambo la kustaajabisha sana kwani nyaraka za Saudi Arabia zinathibitisha kwamba, kabla ya vita vya mwaka 1967, Riyadh iliipa baraka zote Israel ya kushambulia ardhi za nchi za Kiarabu na kuzikalia kwa mabavu.

Matukio ya hivi sasa ya eneo la Mashariki ya Kati nayo yanazidi kuziamsha fikra za walimwengu kuliko wakati mwingine wowote kutokana na walimwengu kuona wazi namna Israel na Saudi Arabia zinavyoshirikiana kuendesha mashambulizi dhidi ya nchi za Kiarabu. Juhudi za waziwazi za Saudia za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni zinafanyika katika hali ambayo kwenye miaka ya hivi karibuni, mbali na Israel kuwakandamiza vibaya Wapalestina na kuendelea kuteka ardhi zao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, inaendelea pia kuzikalia kwa mabavu ardhi nyingine za Kiarabu-Kiislamu. Saudia ndiye kiranja wa juhudi za mapatano baina ya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel na kila siku inafanya njama za kila namna ikiwa ni pamoja na kutangaza wazi uadui wake na mataifa mengine ya Kiarabu na Kiislamu ili kuficha jinai na njama zake za kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel.

Saudia inafanya jinai za kutisha nchini Yemen lakini madola ya Magharibi yamesimama wima kutetea jinai hizo

 

Miongoni mwa njama hizo za Saudia ni mpango wake wa kuitambua rasmi Israel uliopendekezwa na Riyadh mwaka 2002. Mpango huo wa Saudia ulipuuza haki nyingi na za kimsingi za Wapalestina ndio maana umeshindwa. Vile vile njama za Saudi Arabia na Israel za kujaribu kuivunja nguvu kambi ya muqawama na pia kuunga mkono kwao magenge ya kigaidi katika eneo hili, zimezidi kufichua muundo wao halisi  wa kwamba madola hayo mawili ndiyo tishio la kweli la amani, usalama na utulivu wa kimataifa.

Tags