Matokeo ya sera za kigaidi za utawala wa Saudia nchini Yemen
Wizara ya Ulinzi na Kamandi Kuu ya Vikosi vya Majeshi ya Yemen zimetoa taarifa na kutangaza kuwa, jinai ya hivi karibuni ya Saudia ya kumuua kigaidi Saleh al Sammad, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, ni jinai ambayo itapata jibu kali sana.
Kiongozi wa Baraza Kuu la Kisiasa Yemen, Saleh al-Sammad aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za Saudia Arabia katika mkoa wa al-Hudydah. Al-Sammad, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Ansarullah, aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za Saudia siku ya Alkhamisi. Katika siku za hivi karibini mamia ya Wayemen wameuawa katika hujuma zisizo na kikomo za Saudia dhidi ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu. Aidha muungano unaoongozwa na Saudia mbali na kufanya mauaji ya umati, pia unandelea kuiwekea Yemen mzingiro wa angani, ardhini na baharini na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa kitovu cha shari za utawala wa Saudi Arabia na hasa mrithi wa kiti cha ufalme nchini humo, Mohammad bin Salman, ambaye ndie muandaaji wa vita dhidi ya Yemen.
Ikumbukwe kuwa mwezi Machi 2015, Saudi Arabia ilianzisha vita vikubwa vya kivamizi dhidi ya nchi masikini ya Kiarabu ya Yemen kwa baraka kamili za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu. Hadi sasa Wayemen zaidi ya elfu 14,000 wameshauawa huku malaki ya wengine wakijeruhiwa katika hujuma hiyo ya Yemen. Aidha mamilioni ya Wayemen wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na vita hivyo vya Saudia.
Wakati walipoanzisha uvamizi huo, wavamizi hao wa Yemen walikuwa na ndoto za kuvimaliza muda mfupi sana vita hivyo, hata hivyo uvamizi huo umeingia katika mwaka wake wa nne hivi sasa na bado Saudia imeshindwa kufikia malengo yake ndio maana inamalizia hasira zake kwa kushambulia maeneo ya raia baada ya kuona jeshi la Yemen na vikosi vya kujitolea vya wananchi vimezidi kuwa na nguvu na vinaendelea kuyapiga kwa makombora maeneo ya Saudi Arabia hata mji mkuu wake Riyadh.
Hatua ya utawala wa Aal Saudi ya kumuua kigaidi Saleh al-Sammad ina lengo la kuwalenga viongozi wa harakati ya mapambano na muqawama nchini Yemen na hivyo kudhoofisha harakati ya mapambano ya wananchi wa Yemen. Aidha kitendo cha utawala wa Saudia cha kumuua shahidi al-Sammad ni jambo linaloweka wazi utambulisho wa kigaidi wa utawala huo wa Riyadh ambao pia ni chanzo cha makundi ya magaidi wakufurishaji katika uga wa kimataifa.
Ugaidi wa utawala wa Saudia dhidi harakati ya mapambano ya Answarullah ni mfano wa wazi wa kuuiga utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umekuwa ukiwaua viongozi wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina. Nukta hiyo inaashiria ushirikiano wa karibu wa nyuma ya pazia baina ya Saudia na Israel kwa lengo la kuwaangamiza viongozi wa harakati za muqawama au mapambano katika eneo hili. Nukta inayopaswa kuzingatiwa hapa ni kuwa, utawala wa Saudia unauiga kikamilifu utawala wa Kizayuni katika vitendo vyake vya kigaidi na hili linaonyesha kina kirefu cha ushirikiano wa tawala hizo mbili za shari na zilizoshindwa katika jinai zao.
Hivi karibuni, televisheni ya Al Mayadeen ilitangaza kuwa: "Baada ya Saudia kufeli katika mikakati yake ya eneo hili, sasa imejielekeza upande wa utawala wa Kizayuni ili kuunda muungano wa kutoa pigo kwa harakati za mapambano au muqawama. Lakini ushirikiano huo pia nao hautafanikiwa katika kusitisha msururu kwa kushindwa Wasaudi katika eneo. Ali Murtadha, ripoti wa Televisheni ya Al Mayadeen anasema hivi kuhusu jitihada za Saudia kujikurubisha kwa Israel. "Pengine sera za Saudia katika eneo hili ndiyo sababu ya mabadiliko katika fikra za watawala wa Riyadh ambao sasa wamekubali kuwa na uhusiano mpana na Israel. Itwapo tutaangalia kipindi cha kabla ya Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud, tutaona Saudia ilishiriki katika mashambulio mapana zaidi ya kigaidi dhidi ya Syria. Pamoja na hayo njama hiyo ya kutoa pigo kwa Syria iligonga mwamba na hivyo Wasaudia wakaondoka Syria na kuelekeza njama zao nchini Yemen mwaka 2015 lakini hadi sasa hawajaweza kufikia malengo yao katika vita hivyo bali hata vimekuwa na taathira hasi kiasi kwamba hata mji mkuu wa Saudia sasa umekuwa ukilengwa kwa makombora ya balestiki ya Wayemen.
Katika kufuatilia malengo yake ya kigaidi nchini Yemen, Saudia imeanzisha vita vya kipropaganda dhidi ya watu wa nchi hiyo ili kuzusha fakachi na mifarakano baina ya wananchi na harakati ya mapambano kwa kueneza uvumi na uchuku kuhusu kilichopelekea kuuawa Saleh al Samad. Lengo la uzushi huo ni kupotosha fikra za umma kuhusu jinai yake hiyo.
Lakini kuwa macho wananchi na wakuu wa Yemen kuhusu sera za ugaidi na fitina za Saudia ni ishara ya kufeli tena uchochezi wa Riyadh unaofanywa kwa lengo la kubadilisha mlingano katika vita dhidi ya Yemen sambamba na kuzidi kutumbukia wakuu wa Saudi Arabia katika kinamasi walichojichimbia wenyewe huko nchini Yemen.