Muungano wa Marekani wafanya maauaji mengine ya umati nchini Syria
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani ambao unadai kupambana na magaidi wa Daeshi (ISIS) nchini Syria umefanya mauaji mengine ya umati dhidi ya raia wa mashariki mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Shirika la habari la Associated Press limeinukuu duru moja iliyoshuhudia kwa karibu jinai hiyo ikisema kuwa, raia 30 wameuliwa kwa umati jana Alkhamisi baada ya muungano unaoongozwa na Marekani kufanya mashambulizi ya anga katika eneo la al Qasr, mkoani al Hasaka, mashariki mwa Syria. Wengi wa raia hao waliouliwa kwa umati na ndege za Marekani ni wanawake na watoto wadogo.
Kwa mujibu wa shirika hilo la habari, raia wengine wasiopungua 20 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyosababisha hasara kubwa kwa nyumba za raia.
Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ilimuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa hivi sasa wa Baraza la Usalama la umoja huo kulalamikia jinai zinazofanywa na muungano huo unaoongozwa na Marekani, za kuua wananchi wasio na hatia huko Syria.
Itakumbukwa kuwa Marekani na muungano wake huo umevamia na unaendelea kufanya mashambulizi ndani ya ardhi ya Syria tangu mwezi Agosti 2014 bila ya idhini ya serikali ya nchi hiyo na kinyume kabisa na matakwa ya Umoja wa Mataifa. Hadi hivi sasa muungano huo vamizi umeshaua idadi kubwa ya raia wasio na hatia wa Iraq na Syria kwa madai ya eti kupambana na genge la kigaidi la Daesh ambalo limeundwa na hiyo hiyo Marekani.