Serikali ya Sudan yaendela kushinikizwa kuwarejesha nyumbani wanajeshi wake wanaouawa Yemen
Muungano mpya nchini Sudan unaojulikana kwa jina la "Harakati ya Umoja wa Kitaifa" umeitaka serikali ya nchi hiyo iwarejeshe nyumbani wanajeshi iliowatuma nchini Yemen.
Mkuu wa muungano huo, Ghazi Salahuddin amesema, muungano huo umemuandikia barua ya wazi Rais Omar al Bashir na bunge la Sudan ukiwataka wawaondoe mara moja wanajeshi wa nchi hiyo walioko Yemen.
Mashinikizo hayo yamekuja kutokana na idadi ya wanajeshi wanaouawa na kupotea nchini Yemen ikizidi kuongezeka.
Kwa upande wake, Mohammad Issa Aliou, Katibu Mkuu wa harakati hiyo ameilaumu serikali ya Omar al Bashir kwa kuvitenga vyama vingine vya siasa katika maamuzi muhimu ya nchi ikiwa ni pamoja na masuala ya bajeti, kutumwa raia wa nchi maeneo ya vita kama huko Yemen, kufanyiwa marekebisho Baraza la Mawaziri n.k, licha ya upinzani mkali unaooneshwa na vyama hivyo.
Mwezi Machi 2015 serikali ya Rais Omar al Bashir wa Sudan ilikubali kujiunga na muungano wa Saudi Arabia kufanya jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya raia wasio na hatia huko Yemen. Sudan imetuma takriban wanajeshi elfu nne katika vita vya kivamizi nchini Yemen.