Mashambulizi mapya ya anga ya US yaua raia 12 nchini Syria
Mashambulizi mapya ya anga yaliyofanywa na ndege za kijeshi za Marekani yameua raia wasiopungua 12 na kujeruhi wengine wengi katika mkoa wa Hasakah, kaskazini mashariki mwa Syria.
Hujuma hiyo ya jana dhidi ya jengo la makazi ya watu katika eneo la Tal Shayr imefanyika siku moja baada ya mashambulizi mengine ya anga ya ndege za Marekani kuua wakimbizi 18 raia wa Iraq katika kitongoji cha Khuweibra katika mkoa huo huo wa Hasakah.
Ukatili huo wa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Marekani umefanyika siku chache baada ya Rais Bashar al Assad wa Syria kusema kuwa, madola ya Magharibi hayawezi kuiainishia nchi hiyo mustakbali wake na kusisitiza kuwa, wanajeshi wa Uingereza na Marekani walioko nchini humo ni wavamizi.
Nchi hizo za kibeberu zimetuma wanajeshi wao vamizi nchini Syria kwa madai ya kupambana na ugaidi katika hali ambayo kwa mujibu wa ripoti rasmi, Marekani na Uingereza ndio waanzilishi na waungaji mkono wakuu wa magenge ya kigaidi katika eneo hili ikiwemo Syria.
Mapema mwezi huu, muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani wa eti kupambana na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) ulikiri kupitia ripoti kuwa tangu yalipoanza mashambulio ya anga ya muungano huo mwaka 2014 hadi sasa, raia 892 wameuawa katika nchi za Syria na Iraq.
Muungano huo vamizi umeshafanya mashambulio ya anga zaidi ya 29,000 ndani ya ardhi za Syria na Iraq.