Jun 21, 2018 07:34 UTC
  • Human Rights Watch: Saudia inawatia nguvuni watetezi wa haki za binadamu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelaani hatua ya Saudi Arabia ya kuwatia nguvuni wanaharakati wa kutetea haki za wanawake na kusisitiza kuwa, kamatakamata hiyo inafanyika katika wimbi la hivi karibini la kukabiliana na watetezi wa haki za binadamu.

Taarifa iliyotolewa na Human Rights Watch imesema kuwa, serikali ya Saudi Arabia imemtia nguvuni mwandishi na mwanaharakati wa kike, Nauf Abdul Aziz baada ya kutangaza uungaji mkono wake kwa wanaharakati wenzake saba waliotiwa nguvuni nchini humo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Saudia pia imemtia nguvuni mwanaharakati Mayya al Zahrani baada ya kuchapisha risala ya Nauf Abdul Aziz katika mitandao ya kijamii na kwamba wanaharakati hao wanazuiwa kukutana na kuwasiliana na ndugu na jamaa zao.

Human Rights Watch pia imesema serikali ya Saudi Arabia imewazuia baadhi ya wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kufanya safari nje ya nchi. Imesema Riyadh inatumia vibaya Mahakama ya Jinai na Sheria ya Kupambana na Ugaidi kuwahukumu watetezi wa haki za binadamu, waandishi na wakosoaji wa serikali.

Sarah Leah Whitson

Mkurugenzi Mtendaji wa Human Rights Watch kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, Sarah Leah Whitson, amesema Saudi Arabia haiwapi raia wake hata uhuru wa kuwaunga mkono watetezi wa haki za binadamu wanaoshikiliwa jela na amewataka waitifaki wa Magharibi wa Saudia kuishinikiza Riyadh ili iwaachie huru wanaharakati hao tena bila ya masharti yoyote.

Tags