Aug 23, 2018 15:05 UTC
  • Matamshi ya waziri wa Saudia ya kuitetea Israel yazidi kulaaniwa

Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Maulamaa wa Muqawama na msemaji wa harakati ya Answarullah ya Yemen wamelaani vikali matamshi ya waziri wa wakfu wa utawala wa ukoo wa Aal Saud huko Saudi Arabia aliyeutetea na kuukingia kifua wazi wazi utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waziri wa wakfu wa Saudi Arabia, Abdul Latif Aal al Sheikh alidai jana kwamba kamwe Waisrael  hawajawazuia Wapalestina kwenda kutekeleza ibada tukufu ya Hija.

Waziri huyo wa Saudia alikwenda mbali zaidi na kufikia hadi kuiita Israel kuwa ni nchi, ikiwa ni kutangaza rasmi uungaji mkono wake wa kuporwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Sheikh Maher Hamoud, Mkuu wa Umoja wa Kimataifa ya Maulamaa wa Muqawama

 

Matamshi hayo ya waziri wa wakfu wa Saudi Arabia ya kwamba Wazayuni hawajawahi kuwazuia Wapalestina kutekeleza ibada tukufu ya Hija yametolewa katika hali ambayo Israel imewafungia njia zote Wapalestina wa Ghaza za kuingia na kutoka katika eneo hilo.

Shirika la habari la Fars leo Alkhamisi limemnukuu Sheikh Maher Hamoud, Mkuu wa Umoja wa Kimataifa ya Maulamaa wa Muqawama akilaani vikali matamshi ya waziri huyo wa Saudia na kusema kuwa, sehemu kubwa ya Waislamu na Waarabu leo hii wamegundua namna Saudi Arabia inavyofanya kila njia kuweka uhusiano wa kawaida kati yake na adui Israel.

Muhammed Abdul Salaam, msemaji wa harakati ya Answarullah ya Yemen

 

Kwa upande wake, msemaji wa harakati ya Answarullah ya Yemen, Muhammed Abdul Salaam amesema, hakuna kitu chochote kinachoweza kuhalalisha matamshi hayo ya hatari sana ya waziri wa wakfu wa Saudi Arabia.

Vile vile matamshi ya waziri huyo wa Saudia yamelaaniwa vikali sana na watumiaji wa mitandao ya kijamii. Hata hivyo wizara ya mambo ya nje ya Israel imemsifu sana waziri huyo wa Saudi Arabia kwa matamshi yake hayo.

Tags