Mamlaka ya Ndani Palestina: Marekani inapotosha historia ya Quds
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48143-mamlaka_ya_ndani_palestina_marekani_inapotosha_historia_ya_quds
Msemaji wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa matamshi ya Jared Kushner ambaye ni msaidizi na mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani ni jitihada za kupotosha historia ya Palestina hususan ya mji wa Quds (Jerusalem) na maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 14, 2018 23:59 UTC
  • Mamlaka ya Ndani Palestina: Marekani inapotosha historia ya Quds

Msemaji wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa matamshi ya Jared Kushner ambaye ni msaidizi na mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani ni jitihada za kupotosha historia ya Palestina hususan ya mji wa Quds (Jerusalem) na maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo.

Nabil Abu Rudeina amesema kuwa matamshi yaliyotolewa na Jared Kushner katika mahojiano yake ya gazeti la New York Times yanaonesha jinsi anavyotaka kupotosha uhakika kuhusu Palestina na hakuna mazungumzo yatakayofanyika isipokuwa katika msingi wa sheria na maazimio ya kimataifa. Abu Rudeina amesisitiza kuwa Quds (Jerusalem) itaendelea kuwa mji mkuu wa taifa la Paletina. 

Ameongeza kuwa, kuendelea kukana uhakika wa kihistoria na kidini wa watu wa Palestina kunachochea moto wa machafuko na ghasia, na Wapalestina kamwe hawatasalimu amri mbele ya mashinikizo, vikwazo na siasa za kibabe za Marekani. 

Msemaji wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, mienendo ya Marekani inatokana na sera zake za kupendelea kibubusa upotoshaji wa Israel na unaonesha kushindwa na kufeli kwa mienendo hiyo.

Trump, Kushner na Netanyahu

Katika mahojiano yake na gazeti la New York Times, Jared Kushner alidai kuwa Wapalestina wanastahiki kukatiwa misaada ya kibinadamu kwa sababu eti ya kuidharau serikali ya Marekani.  

Marekani imesimamisha misaada yake ya kifedha kwa Wapalestina ikiwemo misaada ya hospitali za Quds na ya Wakala wa Umoja wa Mataifa kwa Ajili ya Wakimbizi na Ajira kwa Wapalestina (UNRWA).