Israel yamzuia Ahed Tamimi binti wa Kipalestina mwanamapambano kuelekea Iran
Baba wa Ahed Tamimi, binti mwanamapambano wa Kipalestina amesema kuwa, licha ya utawala haramu wa Kizayuni kumzuia Ahed kufanya safari, binti yake huyo pamoja na familia yake anaendelea kufanya juhudi kwa ajili ya kusafiri kuelekea Jordan na kisha kutoka hapo kuelekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ili kuendelea na harakati zake kwa ajili ya taifa la Palestina.
Ahed Tamimi ambaye kwa sasa amekuwa nembo ya muqawama katika ardhi za Palestina, alikuwa amekusudia kuondoka Palestina kuelekea Iran kwa ajili ya kuitikia mwaliko wa Mkuu wa Kitengo cha Ng'ambo cha Shirika la Habari la Jamhuri ya Kiislam ya Iran IRIB, wa kushiriki marasimu ya kumtunuku tuzo. Hata hivyo utawala haramu wa Kizayuni ulimzuia kuodoka hapo tarehe saba ya mwezi huu. Bassim al-Tamimi, baba wa binti huyo ameuambia mtandao wa habari wa Misri wa Akhbar al-Youm kwamba, awali familia ya Ahed ilikusudia kufanya safari kuelekea Ulaya na nchi za Kiarabu kwa ajili ya kushiriki shughuli zinazohusiana na muqawama wa Palestina na pia kuelezea tajriba ya binti yake ya kukaa jela kwa kipindi cha miezi minane. Hata hivyo utawala wa Kizayuni uliizuia familia hiyo saa chache kabla ya kuondoka Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kudai kwamba hawataruhusiwa kusafiri hadi kutakapotolewa taarifa nyingine.
Bassim ameongeza kuwa, viongozi wa utawala huo bandia hawakuwaeleza sababu ya zuio hilo, na kwamba licha ya hatua hiyo Ahed Tamimi anaendelea na juhudi za kufanikisha safari yake ya kuingia Jordan na kisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kushiriki harakati hizo za Kipalestina. Itakumbukwa kuwa askari wa utawala katili wa Kizayuni walimkamata Ahed, tarehe 19 Septemba mwaka jana kwa tuhuma za kumshambulia askari wa utawala huo vamizi, huku akiachiliwa huru tarehe 29 Julai mwaka huu, ikiwa ni baada ya kubakia jela kwa miezi minane. Awali msichana huyo mwenye umri wa miaka 17 na ambaye amegeuka kuwa nembo ya muqawama, alielezea uwezekano wa kusafiri nchini Iran kwa kusema, licha ya vizuizi vingi vya Israel vinavyomzuia kuelekea Iran likiwemo tishio la kumrejesha jela, lakini Tela Aviv haiwezi kuzuia malengo yake ya kimuqawama.