Nov 22, 2018 02:39 UTC
  • Kukosolewa siasa za Saudi Arabia zilizo dhidi ya haki za binadamu

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limekosoa vikali kutiwa mbaroni watu nchini Saudi Arabia na kuteswa wanaharakati wa haki za binadamu katika magereza ya nchi hiyo.

Ukosoaji huo wa Amnesty International umetolewa kufuatia kuendelea kamatakamata na mashinikizo ya utawala wa Saudi Arabia dhidi ya wapinzani na wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu.

Ripoti ya Amnesty International na Human Rights Watch inaonyesha kuwa, wanaharakati wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia wakiwemo wanawake kadhaa wamekuwa kizuizini tangu mwezi Mei mwaka huu na wamekuwa wakifanyiwa kila aina ya utesaji na udhalilishaji, ukiwemo unyanyasaji wa kingono, kuadhibiwa kwa mshtuko wa umeme na hata kupigwa mijeledi.

Hatua za utawala wa Aal-Saud za kuwakandamiza wapinzani na wanaharakati wa masuala mbalimbali kama ya kijamii na kiutamaduni, zimeigeuza nchi hiyo na kuifanya kuwa moja ya vituo vya ukiukwaji wa haki za raia katika uga wa kimataifa, kiasi kwamba, akthari ya asasi na jumuiya za kieneo na kimataifa zilizo amilivu katika uga wa haki za binadamu zimejitokeza na kukosoa siasa hizo za Saudi Arabia.

Vikoai vya usalama Saudia vinatuhumiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wapinzani

Asasi hizo zinataka kusitishwa kutiwa mbaroni kiholela raia na vilevile kukomeshwa vitendo vya utesaji na mashinikizo dhidi ya wanaoshikiliwa kizuizini.Yahya al-Asiri, Mkuu wa Jumuiya ya Kutetea Haki za Binadamu nchini Saudi Arabia anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Njia pekee ya kusitishwa uhalifu wa utawala wa Aal-Saud ni kushinikizwa utawala huo. Mashinikizo hayo hayawezi kuwa ni kutoka ndani ya Saudia kwa sababu nchini humo kuna mbinyo, na ukandamizaji ni wa kutisha mno. Watu wote ambao walipaza sauti na kuukosoa utawala wa Saudia ndani ya nchi hiyo hivi sasa wanasota jela.

Utawala wa Riyadh hauendeshi siasa za vitisho ndani ya nchi hiyo tu, bali hata nje ya nchi, kwani wapinzani wa utawala wa ukoo wa Aal-Saud walioko nje ya nchi hiyo wanakabiliwa na hatari ya kutiwa mbaroni na hata kuuawa. Mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi habari na mkosoaji wa Saudia yaliyofanyika ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul Uturuki ni mfano wa wazi wa siasa za Riyadh zilizo dhidi ya ubinadamu.

Jinai za Saudi Arabia nchini Yemen

Kuanzisha vita vya Yemen na kuuawa na kujeruhiwa maelfu ya raia hususan wanawake na watoto wadogo kufuatia mashambulio ya mabomu ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ni mfano mwingine wa viongozi wa Saudia kutoheshimu haki za binadamu. Moja ya jinai za kutisha ni shambulio la muungano vamizi  huko Yemen chini ya uongozi wa Saudia tarehe 9 mwezi Agosti mwaka huu dhidi ya basi lililokuwa limebeba watoto wa Kiyemeni katika mji wa al-Dhahyan mkoani Sa'ada lililoua zaidi ya watoto 50. 

Kuendelea mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, kumeifanya nchi hiyo ikabiliwe na uhaba mkubwa wa chakula na dawa, kiasi cha kuzifanya asasi na jumuiya za kimataifa zitahadharishe juu ya uwezekano wa kutokea mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu katika nchi hiyo. Himaya na uungaji mkono wa nchi nyingine zinazokiuka haki za binadamu kama Bahrain na  kushirikiana nazo, ni upande mwingine wa sarafu wa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal-Saud.

Marekani imekuwa ikifaidika kifedha kwa kuiuzia silaha Saudi Arabia, hivyo haiko tayari kukosoa jinai za Riyadh 

Katika hali ambayo, wananchi wa Bahrain wameanzisha harakati na maandamano ya amani wakitaka uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi, utawala wa Manama ukipata msaada wa kijeshi wa Saudi Arabia na maafisa wa kijeshi wa Imarati, umekuwa ukikandamiza vikali maandamano ya amani ya wananchi hao.

Licha ya kuweko ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu ndani ya Saudi Arabia na hata kuendelea siasa hizo za mkono wa chuma za Riyadh nje ya nchi, lakini inaonekana kuwa, Marekani na washirika wengine wa Riyadh wangali wanafanya kila liwezekanalo ili kulinda biashara yao chafu ya kuiuzia Saudia silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola. Hatua ya madola hayo, si tu kwamba, imepuuza jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na Saudi Arabia, bali mataifa hayo  yamekuwa hayasiti hata kidogo kuiunga mkono nchi hiyo ya Kiarabu kwa siri na kwa dhahiri.

Tags