UN yapinga vikali mashambulizi ya Wazayuni wa Israel huko Quds
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i51166-un_yapinga_vikali_mashambulizi_ya_wazayuni_wa_israel_huko_quds
Nickolay Mladinov ambaye ni mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Mashariki ya Kati amesema kuwa mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya kijiji cha kaskazini mwa Quds (Jerusalem) hayakubaliki na yanashtua sana.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 28, 2019 07:36 UTC
  • UN yapinga vikali mashambulizi ya Wazayuni wa Israel huko Quds

Nickolay Mladinov ambaye ni mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Mashariki ya Kati amesema kuwa mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya kijiji cha kaskazini mwa Quds (Jerusalem) hayakubaliki na yanashtua sana.

Wazayuni wa Israel wamezidisha mashambulizi yao huko Baitul Muqaddas katika mwaka huu mpya wa 2019 sambamba na duru mpya ya harakati za Marekani za kutaka kuzindua na kutekeleza njama ya Donald Trump iliyopewa jina la "Muamala wa Karne". Kwa utaratibu huo Baitul Muqaddas sasa imekuwa uwanja wa kutunisha misuli wa askari na walowezi wa Kizayuni wanaotaka kuharibu utambulisho wa Kiislamu wa mji huo mtakatifu.

Tunapotazama hali ya Palestina baada ya Rais Donald Trump kushika madaraka ya nchi huko Marekani tunaona kuwa, hujuma na mashambulizi ya Israel na walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina yameshadidi zaidi chini ya kivuli cha sera za Trump za kuunga mkono kikamilifu siasa za kibaguzi za serikali ya Tel Aviv. Siasa hizo za kuimarisha ubeberu wa Israel zimeambatana ya harakati za Marekani za kuimarisha majeshi yake katika eneo la Mashariki ya Kati kwa shabaha ya kuzusha woga na hofu kati ya nchi za eneo hilo na kuzilazimisha zikubali mpango wa Muamala wa Karne. Moja kati ya vipengee vikuu vya mpango huo ni maudhui ya Quds, na iwapo utatekelezwa basi Wapalestina watapokonywa kikamilifu eneo hilo takatifu. 

Walowezi wa Kizayuni wakimtesa kijana wa Kipalestina

Ili kufanikisha njama hiyo ya kuwapokonya kikamilifu Wapalestina eneo hilo la Quds, Rais Donald Trump alichukua uamuzi wa kuhamisha ubalozi wa nchi hiyo kutoka Tel Aviv na kuupeleka Quds baada ya kuitambua rasmi kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Sambamba na hayo Israel imekuwa ikifanya juu chini na usiku na mchana kubadilisha sura na utambulisho wa  Kiislamu wa mji huo na kuupa sura ya Kiyahudi. Hatua iliyochukuliwa hivi karibuni na baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu ya kutenga bajeti ya dola bilioni 15 kwa ajili ya kutimiza mpango wa kuiyahudisha kikamilifu Quds tukufu hadi kufikia mwaka 2020 ni sehemu ya harakati za utawala huo za kudumisha sera zake za kivamizi na kibeberu huko Palestina.

Harakati za kutaka kujipanua za Israel huko Quds katika miaka ya hivi karibuni zimeongezeka zaidi ikilinganishwa na miaka ya kabla yake na zinaonesha kuwa, utawala huo ghasibu unatumia nguvu zake zote kwa ajili ya kuudhibiti kikamilifu mji huo.

Hata watoto wa Palestina hawakusalimika...

Quds na moyo wake, yaani Msikiti wa al Aqsa, daima imekuwa ikishambuliwa na Wazayuni wenye misimamo mikali wa Israel. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, tabia ya kupenda kujitanua zaidi ni miongoni mwa sera kuu na misingi ya utawala haramu wa Israel, na vyama na makundi yote ya kisiasa ya utawala huo daima yamekuwa yakifanya jitihada za kuifanya Quds itambuliwe kuwa mji mkuu wa Isarel na kuishawishi jamii ya kimataifa ikubaliane na jambo hilo. Ushirikiano uliopo baina ya makundi mbalimbali ya Israel kuhusu suala hilo unatia nguvu uhakika huo licha ya hitilafu za kisiasa na kimitazamo zinazotawala makundi hayo hususan kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu.

Kwa ujumla inatupasa kusema kuwa, hujuma na harakati za utawala ghasibu wa Isarel dhidi ya Quds na sera zake za kutaka kuuyahudisha mji huo mtakatifu ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yamepiga marufuku harakati yoyote ya kufanya mabadiliko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu likiwemo eneo la Baitul Muqaddas.  

Pamoja na hayo yote, upinzani wa jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa dhidi ya harakati na hujuma za Wazayuni huko Quds ni kielelezo cha kufeli njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kuishawishi jamii ya kimataifa ikubaliane na sera hizo za kutaka kujitanua na kutwaa ardhi zaidi za Palestina.