Jun 09, 2019 03:06 UTC
  • Answarullah: Nchi zinazoishambulia Yemen zinatekeleza jinai zilizoratibiwa kimataifa

Harakati ya Answarullah ya nchini Yemen imetoa radiamali yake kufuatia shambulizi la vibaraka wa Imarati dhidi ya Waislamu waliokuwa wanaswali msikitini katika mkoa wa Ad Dali na kusema kuwa, jinai hiyo ni moja ya jinai zilizoratibiwa kimataifa.

Katika shambulizi la jana la wanamgambo wanaoungwa mkono na Imarati katika msikiti wa mji wa Al Azariq wa mkoa wa Ad Dali, kusini mwa Yemen Waislamu kadhaa waliokuwa wanaswali msikitini hapo waliuawa na wengine kujeruhiwa. Kufuatia jinai hiyo Muhammad Abdussalam, Msemaji wa Harakati ya Answarullah sambamba na kubainisha kwamba shambulizi hilo linaonyesha uchafu wa vita vinavyotekelezwa na nchi zinazoishambulia Yemen, amesema kuwa jinai iliyofanywa na vibaraka wa Imarati kuwalenga watu waliokuwa wanaswali, ni jinai kubwa inayotokana na woga wa wahusika.

Muhammad Abdussalam, Msemaji wa Harakati ya Answarullah

Inafaa kuashiria kuwa Imarati na Saudia zinaendesha harakati zao za kijeshi katika maeneo ya kusini mwa Yemen ambapo zinawatumia vibaraka wao kwa ajili ya kutekeleza jinai na mauaji. Katika siku za hivi karibuni nchi hizo zimeshadidisha mashambulizi katika mkoa wa  Ad Dali, kusini mwa Yemen. Na hii ni kwa sababu vikosi vya serikali ya wokovu wa kitaifa vimefanikiwa kudhibiti maeneo mengi yaliyokuwa mikononi mwa vibaraka hao wa Saudia na Imarati.

Tags