UN: Watoto 7500 wa Kiyemeni wameuawa au kupata ulemavu
Umoja wa Mataifa umeashiria hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili Yemen hivi sasa na kueleza kuwa watoto zaidi ya 7,500 wameuawa au kujeruhiwa nchini humo.
Virginia Gamba, Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya watoto katika hali ya migogoro ametoa ripoti inayoeleza kuwa, hadi kufikia sasa watoto 7,500 wa Kiyemeni wameuawa au kujeruhiwa katika vita dhidi ya wananchi wa Yemen. Bi Gamba ameongeza kusema katika ripoti yake hiyo kwamba, idadi kubwa ya watoto hao wameuawa kwenye mashambulizi ya anga, mapigano ya nchi kavu, kutokana na milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini na mabomu mengine na kwamba mashambulizi dhidi ya shule na hospitali nchini Yemen yangali ni mengi sana na maelfu ya nyumba zimebomolewa.
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu hatari ya kukumbwa na njaa mamilioni ya raia wa Yemen na kueleza kuwa, watoto zaidi ya milioni nane wa nchi hiyo wanashindwa kupata huduma ya maji na wengine milioni mbili wanasumbuliwa na utapiamlo.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, Yemen inakumbwa na mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu kuwahi kushuhudiwa duniani kiasi kwamba idadi ya watu milioni 22 ambayo inaunda asilimia 75 ya jamii ya nchi hiyo wanahitaji misaada mbalimbali ya kibinadamu. Wananchi wa Yemen milioni 4 na laki nne hawajui ni wapi watapata mlo wao wa siku.
Sambamba na maafa haya Rais Donald Trump wa Marekani anaendelea kuuuzia silaha muungano vamizi unaoendesha vita dhidi ya wananchi wa Yemen unaaongozwa na Saudia na Imarati.