Abu Bakr al Baghdadi, Daesh na maafa yaliyosababishwa na kundi hilo
Hatimaye kiongozi wa kundi la kigaidi la Daesh, Abu Bakr al Baghdadi ameangamizwa, na Abdullah Qardash aliyekuwa afisa wa jeshi la Saddam Hussein nchini Iraq ameteuliwa na kundi hilo kuwa kiongozi mpya wa Daesh.
Tunaweza kuandika na kuzungumzia mengi kuhusiana na kundi la Daesh ikiwa ni pamoja na jinsi lilivyoanzishwa na nafasi ya Marekani na waitifaki wake katika kuundwa kundi hilo la kigaidi. Hata hivyo swali muhimu zaidi linalojitokeza ni kwamba, kujitokeza kwa kundi hilo na Abu Bakr al Baghdadi kumeacha athari zipi kwa eneo la magharibi mwa Asia?
Miongoni mwa athari mbaya za kudhihiri al Baghdad na kundi hilo ni maafa ya kibinadamu yaliyofanyika katika nchi zilizovamiwa na kushambuliwa na wapiganaji wa kundi la Daesh. Mwezi Juni mwaka 2014 Abu Bakr al Baghdadi alijitangaza kuwa khalifa wa kundi la Daesh katika eneo la Mosul huko kaskazini mwa Iraq na kudai kuwa, anataka kuanzisha dola la khilafa na utawala wa Kiislamu. Daesh na al Baghdadi walibakia Iraq kwa kipindi cha miaka 4 lakini wamefanya maafa na jinai kubwa katika nchi hiyo ambazo ni nadra sana kutokea katika historia ya mwanadamu. Mauaji ya halaiki ya kambi ya Speicher ni miongoni mwa jinai hizo za kutisha za kundi la Daesh nchini Iraq. Katika jinai hiyo kundi la Daesh liliwaua kwa umati Waislamu 1700 wa kishia waliokuwa wakipata mafunzo katika Kituo cha Anga cha Speicher na kuwazika katika kaburi moja la umati. Wanafunzi hao waliuawa bila ya kuuwa na silaha ya aina yoyote.
Magaidi wa kundi hilo la Daesh pia liliwatumia raia hususan wanawake na watoto kama ngao ya vita ya kujikinga na mshambulizi. Wapiganaji wa kundi hilo pia waliwabaka na kuwauza wanawake wengi wa Iraq na Syria kama watumwa.
Miongoni mwa jinai za kutisha za kundi hilo la Daesh ni kuwachoma moto raia wakiwa hao na kuwakata vichwa kadamnasi na mbele ya halaiki ya watu. Jinai za kutisha za kundi hilo ziliwalazimisha watu wengi hususan wa jamii ya Izadi kukimbia makazi yao na kuelekea maeneo ya milimani ambako wengi miongoni mwao waliaga dunia kwa njaa na hali mbaya ya hewa.
Daesh chini ya uongozi wa al Baghdadi ilivuruga kabisa misingi ya familia katika mikoa iliyokuwa ikidhibitiwa na kundi hilo nchini Iraq, jinai ambayo itakuwa na athari mbaya za muda mrefu kwa Wairaqi. Japokuwa Daesh na Abu Bakr al Baghdadi wameangamia lakini fikra za kundi hilo na mabaki yake yangalipo katika baadhi ya maeneo ya Iraq na uwepo wao umeshuhudiwa katika machafuko ya sasa nchini humo.
Miongoni mwa athari mbaya za kujitokeza kwa Abu Bakr al Baghdadi na kundi la Daesh ni kuharibika muundo wa kijamii katika nchi zilizovamiwa na wapiganaji wa kundi hilo la kitakfiri na kigaidi. Magaidi wa Daesh hususan katika nchi za Iraq na Syria wameharibu kabisa miundombinu ya kijamii zikiwemo nyumba na makazi ya raia, shule, hospitali na vituo vya afya, barabara na sekta ya kilimo. Jinai hizo zimezirudisha nyuma kwa makumi ya miaka nchi kama Iraq na Syria. Hapana shaka kuwa miongoni mwa sababu za mapungufu na huduma mbaya za kijamii zinazoshuhudiwa sasa nchini Iraq ambazo ni miongoni mwa sababu za maandamano na machafuko ya sasa nchini humo ni jinai zilizofanywa na kundi hilo la Daesh katika kipindi cha miaka minne ya uvamizi wake huko Iraq.
Athari nyingine mbaya ya kudhihiri Abu Bakr al Baghdadi na Daesh katika eneo la magharibi mwa Asia ni kudhoofisha serikali kuu katika nchi zilizovamiwa na wapiganaji wa kundi hilo. Sayyid Jawad Salehi ambaye ni mhadhiri na mtafiti wa masuala ya magharibi mwa Asia anaamini kuwa: Jinai zilizofanywa na kundi hilo zimetayarisha mazingira ya kudhoofika serikali kuu katika nchi zilizovamiwa na wapiganaji wa Daesh. Daesh chini ya uongozi wa al Baghdadi ilipewa kipaumbele cha kwanza katika katika mipango ya serikali na tawala za Asia magharibi. Mapambano dhidi ya genge la Daesh yamezigharimu sana nchi za magharibi mwa Asia hususan Iraq na Syria na ambazo zimetumia sehemu kubwa ya mapato na rasilimali watu kwa ajili ya kupambana na kundi hilo.
Mwisho kabisa inatupasa kuashiria kwamba, japokuwa Rais Donald Trump wa Marekani jana alijitokeza hadharani mbele ya vyombo vya habari na kujigamba kwamba nchi hiyo imemuangamiza Abu Bakr al Baghdadi lakini inatupasa kusema kuwa, Daesh ilifanya jinai hizo zote kwa maslahi ya Marekani na waitifaki wake, na kuangamia kwa al Baghdadi si suala muhimu sana kwa nchi za magharibi mwa Asia bali kunahisabiwa kuwa ni kuanza duru na kipindi kipya cha uhai wa kundi hilo.