Shambulizi la anga la Israel laua na kujeruhi Wapalestina Gaza
Mashambulizi ya anga ya ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel yamepelekea kuuawa shahidi raia mmoja wa Palestina na kujeruhiwa wengine wawili.
Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti kuwa, Ahmed al-Shehri aliyekuwa na umri wa miaka 27 ameuawa shahidi katika hujuma hizo zilizofanywa mapema leo na ndege hizo za kijeshi za utawala haramu wa Israel.
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa, mashambulizi hayo yamelenga vituo vya mafunzo vya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kusini mwa mji wa Khan Younis katika Ukanda wa Gaza.
Jeshi la utawala katili wa Israel limedai kuwa limetekeleza mashambulizi hayo ya anga kama jibu kwa shambulizi la maroketi lililofanywa jana na wanamuqawama wa Palestina, wakati wa maandamano ya 'Haki ya Kurejea'.

Tokea Machi 30 hadi sasa Wapalestina zaidi ya 330 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel wakati wakishiriki katika maandamano hayo ya amani ambayo hufanyika kila Ijumaa.
Wakati huohuo, msemaji wa Hamas, Fawzi Barhoum ameuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya chokochoko zake hizo dhidi ya ngome na vituo vya harakati hiyo ya Muqawama katika Ukanda wa Gaza na kubainisha kuwa, "Damu ya taifa letu ina thamani kubwa sana, na hatutamruhusu yeyote kuichezea."