Pakistan: Hatuhitaji uingiliaji kati wa Marekani kutatua masuala yetu na Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i59496-pakistan_hatuhitaji_uingiliaji_kati_wa_marekani_kutatua_masuala_yetu_na_afghanistan
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi amesema, hauhitajiki uingiliaji kati wa Marekani kwa ajili ya kutatuliwa masuala ya pande mbili kati ya nchi yake na Afghanistan.
(last modified 2026-05-06T11:35:21+00:00 )
Mar 02, 2020 03:28 UTC
  • Pakistan: Hatuhitaji uingiliaji kati wa Marekani kutatua masuala yetu na Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi amesema, hauhitajiki uingiliaji kati wa Marekani kwa ajili ya kutatuliwa masuala ya pande mbili kati ya nchi yake na Afghanistan.

Shah Mahmood Qureshi amesisitiza kuwa: Inapasa ifahamike kwamba Pakistan ni jirani wa kudumu wa Afghanistan; na Marekani ndiyo inayopaswa kufikiria mpango wa kuondoa askari wake Afghanistan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameeleza bayana kuwa, ikiwa Islamabad itakuwa na tatizo lolote na Kabul haitaiomba msaada Washington wa kuingilia kati kwa ajili ya kuzipatanisha, bali nchi hizo zenyewe zitafanya mazungumzo ya moja kwa moja baina yao.

Shah Mahmood Qureshi ameongeza kuwa, Pakistan na Afghanistan zinatambua kwamba, mtazamo wa nia njema uko pande zote mbili na kwamba yaliyopita huko nyuma inapasa yawekwe kando na kuangalia mbele.

Marekani na kundi la Taliban zikisaini makubaliano ya amani ya Afghanistan, mjini Doha, Qatar

Kabla ya hapo, Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan alisema, ana matumaini kuhusiana na mkataba wa suluhu uliosainiwa kati ya Taliban na Marekani kwa ajili ya kurejesha utulivu na amani nchini Afghanistan na akasisitiza kuwa, Islamabad itatoa mchango wake kwa ajili ya kufanikisha makubaliano hayo ili kusaidia kurejesha amani nchini humo.

Pakistan na Afghanistan zinatofautiana juu ya masuala kadhaa, ikiwemo uainishaji alama za mipaka, hujuma za kigaidi zinazofanywa na makundi yenye misimamo ya kufurutu mpaka katika maeneo ya mpakani na maroketi yanayovurumishwa kwenye vijiji vya mpaka wao wa pamoja huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kuwa unachochea vitendo hivyo.../