Vibaraka wa Imarati wapigana kusini mwa Yemen
Duru za habari zimeripoti kujiri mapigano makali kati ya wanamgambo vibaraka wa Imarati katika mji wa Aden, kusini mwa Yemen.
Wanamgambo hao vibaraka wa Imarati ambao wana mafungamano na Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen, wameshambuliana na wenzao katika mji wa Aden. Katika mapigano hayo idadi ya wanamgambo hao vibaraka wameripotiwa kujeruhiwa sambamba na kuteketezwa moja ya magari ya kijeshi. Mji wa Aden unaopatikana kusini mwa Yemen, unadhibitiwa na askari wanaoungwa mkono na Imarati. Katika miezi ya hivi karibuni mbali na mapigano ya ndani kati ya askari hao hao, kwa mara kadhaa kumekuwa kukijiri mapigano makali kati ya askari wenye mfungamano na Abdrabbuh Mansur Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na anayeungwa mkono na Saudia.
Wakati huo huo wakazi wa mji huo nao wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara ya kulaani ukatili unaofanywa na askari wa muungano vamizi wa Saudia dhidi ya wakazi wao. Katika uwanja huo mashirika ya kutetea haki za binadaamu yameripoti habari za kuwepo visa vya utekaji nyara watu na kuwafunga katika jela za siri za muungano huo vamizi huko kusini mwa Yemen.