Mamluki wa Saudia na Imarati watishiana vita Yemen
Kundi la watu wanaopigania kujitenga kusini mwa Yemen linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu limetoa onyo kali la kuingia vitani na mamluki wa Saudi Arabia, huku migawanyiko baina ya pande mbili hizo ikiendelea kupanuka.
Kundi hilo linalopigania kujitenga liitwalo Baraza la Mpito la Kusini (STC) limesema tayari limewataarifu mabalozi wa nchi kubwa kadhaa nchini Yemen, pamoja na Mjumbe wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths juu ya uwezekano mkubwa wa kutokea vita baina ya pande mbili hizo.
Kundi hilo linaituhumu serikali ya rais aliyejiuzulu na kukimbia nchi wa Yemen, Abd Rabbuh Mansur Hadi na inayoungwa mkono na Riyadh kuwa inakiuka makubaliano ya kugawana mamlaka iliyosainiwa baina ya pande mbili hizo Novemba mwaka jana.
Jana Jumamosi, mamluki wa Saudia walidai kuwa wamefanikiwa kudhibiti baadhi ya maeneo ya mkoa wa Socotra kusini mwa Yemen, ukiwemo Uwanja wa Kimataifa wa Ndege katika kisiwa hicho, ambayo yalikuwa mikononi mwa Baraza la Mpito la Kusini linaloungwa mkono na Imarati.
Hitilafu kubwa baina ya Riyadh na Abu Dhabi ndani ya muungano vamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen kuhusiana na eneo la kusini mwa nchi hiyo maskini ya Kiarabu zilianza mwaka jana baada ya Imarati kutangaza kuwa, inawaondoa wanajeshi wake nchini Yemen.
Migongano ya Saudia na Imarati huko kusini mwa Yemen na jitihada za kuzidisha satua na ushawishi wa kila mmoja wao, ilidhihirika wazi kutokana na ubabe wa pande mbili hizo uliojitokeza katika maeneo ya Al Mahrah na Socotra.