Msuguano baina na UAE na Saudia washtadi kusini mwa Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i60607-msuguano_baina_na_uae_na_saudia_washtadi_kusini_mwa_yemen
Siku chache baada ya kuvunjika mazungumzo baina ya serikali iliyojiuzulu ya Yemen ya Abdrabbuh Mansur Hadi inayoungwa mkono na Saudi Arabia na Baraza la Mpito la Kusini linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, vibaraka hao wa Imarati wamejitangazia mamlaka ya ndani katika mikoa ya kusini mwa nchi hiyo maskini ya Kiarabu iliyozama kwenye dimbwi la vita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2020 03:17 UTC
  • Msuguano baina na UAE na Saudia washtadi kusini mwa Yemen

Siku chache baada ya kuvunjika mazungumzo baina ya serikali iliyojiuzulu ya Yemen ya Abdrabbuh Mansur Hadi inayoungwa mkono na Saudi Arabia na Baraza la Mpito la Kusini linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, vibaraka hao wa Imarati wamejitangazia mamlaka ya ndani katika mikoa ya kusini mwa nchi hiyo maskini ya Kiarabu iliyozama kwenye dimbwi la vita.

Katika taarifa yake ya mapema leo Jumapili, Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen limejitangazia utawala wa ndani katika maeneo ya kusini mwa Yemen kuanzia saa sita usiku wa kuamkia leo, huku wakiituhumu serikali ya rais mtoro aliyejiuzulu Mansur Hadi kuwa ya kifisadi na yenye usimamizi mbaya.

Mohammed al-Hadhrami, Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala huo wa Hadi amesema tangazo hilo la Baraza la Mpito la Kusini linaashiria kujiondoa kikamilifu kwenye makubaliano ya kugawana mamlaka yaliyosainiwa baina ya pande mbili hizo mwaka jana. Amesema, "Baraza la Mpito litabeba dhima peke yake ya hatari na madhara yatakayosababishwa na tangazo lake hilo."

Wiki iliyopita, baraza hilo linalopigania kujitenga maeneo ya kusini mwa Yemen kwa uungaji mkono wa Imarati lilitoa onyo kali na kutishia kuingia vitani na mamluki wa Saudi Arabia, huku migawanyiko baina ya pande mbili hizo ikiendelea kupanuka.

Makumi ya maelfu wameuawa Yemen tokea 2015 katika mashambulio ya muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia

Hii ni baada ya mamluki wa Saudia kudai kuwa wamefanikiwa kudhibiti baadhi ya maeneo ya mkoa wa Socotra kusini mwa Yemen, ukiwemo Uwanja wa Kimataifa wa Ndege katika kisiwa hicho, ambayo yalikuwa mikononi mwa Baraza la Mpito la Kusini linaloungwa mkono na Imarati.

Hitilafu kubwa baina ya Riyadh na Abu Dhabi ndani ya muungano vamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen kuhusiana na eneo la kusini mwa nchi hiyo maskini ya Kiarabu zilianza mwaka jana baada ya Imarati kutangaza kuwa inawaondoa wanajeshi wake nchini Yemen.