Mazungumzo ya kuondoka jeshi la Marekani nchini Iraq kuanza mwezi Juni
Msemaji wa Mkuu wa Majeshi ya Iraq amesema kuwa, mazungumzo ya jinsi ya kuondoka majeshi ya Marekani katika ardhi ya nchi hiyo yataanza mwezi Juni mwaka huu.
Meja Jenerali Abdul Karim Khalaf amesema kuwa mwezi Juni mwaka huu Baghdad na Washington zitaketi kwenye meza ya mazungumzo ya kupanga jedwali la kuondoka askari wa Marekani nchini Iraq na kwamba nchi yake imeazimia ipasavyo kuwaondoa askari wote wa kigeni katika ardhi ya Iraq wakiwemo Wamarekani.
Meja Jenerali Khalaf amesema Marekani tayari imewaondoa baadhi ya wanajeshi wake nchini Iraq na kwamba mazungumzo yajayo yatajadili jinsi ya kuondoka kikamilifu askari wa nchi hiyo.

Mapema mwezi huu wa Aprili aliyekuwa kaimu waziri mkuu wa Iraq, Adil Abdul Mahdi alitangaza kuwa, tarehe 10 na 11 mwezi Juni pande hizo mbili zitakutana kujadili kadhia ya kuondoka askari wote wa Marekani katika ardhi ya Iraq.
Mwanzoni mwa mwaka huu Bunge la Iraq lilipasisha sheria ya kuwafukuza wanajeshi wote wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo. uamuzi huo ulichukuliwa baada ya jeshi gaidi la Marekani kumuua aliyekuwa kamanda wa jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran Luteni Jenerali Qassem Soleimani akiwa pamoja na kaimu mkuu wa kikosi cha wapiganaji wa kujitolea cha al Hashdul Shaabi Abu Mahdi Al Muhandes karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo.