Uturuki: Taarifa ya nchi tano dhidi yetu imetumia vipimo vya kiundumakuwili
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesema, taarifa ya pamoja iliyotolewa na Misri, Ugiriki, Imarati, Ufaransa na Cyprus kuhusu Bahari ya Mediterania inaonyesha vipimo vya kiundumakuwili vinavyotumiwa na nchi hizo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeeleza kuwa, taarifa ya pamoja ya mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Ugiriki, Imarati, Ufaransa na Cyprus kuhusu Bahari ya Mediterania inaonyesha vipimo vya undumakuwili zinavyotaka kutumia nchi hizo na ikazitaka nchi zilizosaini taarifa hiyo zichukue hatua kimantiki na kulingana na sheria za kimataifa na kusisitiza kuwa uthabiti katika eneo hautopatikana isipokuwa kwa kutumia njia ya mazungumzo na kwa ushrikiano wenye uwazi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeongeza kuwa, taarifa ya pamoja ya nchi hizo tano imetolewa baada ya Ankara kuzima na kufelisha sera haribifu za nchi hizo dhidi ya uthabiti katika eneo na uungaji mkono wao kwa watu waliotaka kufanya jaribio la mapinduzi.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesisitiza kuwa, kuwepo uadui dhidi ya Uturuki ndio sababu ya kushiriki Imarati katika kusaini taarifa ya nchi hizo tano ilhali nchi hiyo haina uhusiano wowote na Bahari ya Mediterania na kwamba faili la uhalifu uliofanywa na Abu Dhabi dhidi ya Uturuki na Libya linajulikana vizuri.
Misri, Imarati, Ufaransa, Ugiriki na Cyprus zilitoa taarifa ya pamoja jana usiku ya kulaani kile zilichokitaja kuwa ni uingiliaji kijeshi wa Uturuki nchini Libya na zikaitaka serikali ya Ankara isitishe kupeleka askari wake nchini humo.
Katika taarifa yao hiyo, nchi hizo tano zimelaani pia harakati zinazofanywa na Uturuki karibu na pwani ya Cyprus.../