Sayyid Hassan Nasrallah abainisha nafasi ya leo ya harakati ya muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i61250-sayyid_hassan_nasrallah_abainisha_nafasi_ya_leo_ya_harakati_ya_muqawama
Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu MKuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amefanya mahojiano kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 20 wa kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon ambalo lilikuwa limekaliwa kwa mabavu na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel. Jeshi hilo la Kizayuni lililazimika kuondoka kwa madhila kusini mwa Lebanon mnamo Mei 25 mwaka 2000.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 27, 2020 21:51 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrallah abainisha nafasi ya leo ya harakati ya muqawama

Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu MKuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amefanya mahojiano kwa mnasaba wa maadhimisho ya mwaka wa 20 wa kukombolewa eneo la kusini mwa Lebanon ambalo lilikuwa limekaliwa kwa mabavu na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel. Jeshi hilo la Kizayuni lililazimika kuondoka kwa madhila kusini mwa Lebanon mnamo Mei 25 mwaka 2000.

Katika mahojiano yake, Sayyid Hassan Nasrallah ameashiria matukio muhimu ya kieneo. Amesema Hizbullah imepata nguvu zaidi ya ilivyokuwa mwaka  2000 huku utawala wa Kizayuni wa Israel nao ukizidi kudhoofika. Kuna ishara kadhaa kuhusiana na kupata nguvu Hizbullah na kudhoofika Israel.

Ishara ya kwanza ni vita vya mwaka 2006 vya Israel na Hizbullah ambavyo viliibua muelekeo mpya katika matukio ya eneo la Asia Magharibi. Katika vita hivyo, nguvu za makombora na intelijensia za  Hizbullah zilionyesha kuwa ile ngano ya kutoshindwa Israel imesambaratika kwani katika vita hivyo Israel ilishindwa na kundi na wala si nchi ya Kiarabu.

Ishara ya pili ya kudhoofika Israel ni kuwa, tokea mwaka 2006 hadi sasa, haijathubutu kuingia vitani na Hizbullah kwani inafahamu vyema kuwa, iwapo itaanzisha vita basi haitakuwa na uwezo wa kuvimaliza. Kama alivyosema Sayyed Hassan Nasrallah, moyo wa kimapambano wa Hizbullah ungali pale pale katika hali ambayo Israel imepoteza moyo na motisha wa kupigana na Hizbullah.

Ishara ya tatu ni kuwa, kwa mtazamo wa nguvu za kijeshi, Hizbullah imeimarika kwa kiasi kikubwa. Kuhusiana na nukta hii, Sayyed Hassan Nasrallah anasema: "Hizbullah hivi sasa ina zana na uwezo mkubwa wa kivita ambao haikuwa nao kabla ya mwaka 2000 na hata wanafikra na wachambuzi wa utawala wa Kizayuni wanakiri kuhusu nukta hii.

Wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon

Ishara ya nne ni kuwa,  mhimili wa muqawama katika eneo leo hauishii tu katika Hizbullah ya Lebanon bali kunashuduiwa ongezeko la makundi ya muqawama na mapambano ya Kiislamu. Pia hali ya Palestina si kama ilivyokuwa mwaka 2000.

Sayyid Hassan Nasrallah anafafanua nukta hiyo na kusema: "Leo mapambano yanazidi kuimarika Lebanon na Palestina ikijumuisha Ukanda wa Ghaza. Kwa mfano  Ghaza ambayo mwaka 2000 ilikuwa inakaliwa kwa mabavu leo iko huru na makundi ya Palestina katika eneo hilo yana uwezo wa makombora ambayo yanaweza kulenga miji yote ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (yaani Israel).

Nukta nyingine ya mahojiano ya Sayyid Hassan Nasrallah ni sisitizo lake kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni utawala wa Kibaguzi. Hakuna shaka kuwa, utawala wa Kizayuni ni nembo ya ubaguzi wa rangi duniani kwa sababu si tu kuwa utawala huo hauamini misingi yoyote ya ubinadamu, bali hata unadai kuwa Mayahudi ni kaumu bora na ni kwa msingi huo ndio Wazayuni wakatekeleza mpango wa kuyahudisha mji wa Quds (Jerusalem) na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu. Kwa msingi huo, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah anaamini kuwa, utawala wa Israel si dola la  Kiyahudi wala la kidini kwani serikali ambayo ina historia ya kutekeleza mauaji haiwezi kuwa serikali ya kidini."

Nukta nyingine katika mahojiano ya Kaitbu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ni kuhusu sababu ya uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo. Marekani ina idadi kubwa ya majeshi katika eneo la Asia Magharibi na hata imekataa kuondoa majeshi yake Iraq pamoja na kuwa Wairaqi wanasisitiza majeshi hayo ajinabi yaondoke. Sababu kuu ya kuwepo majeshi ya Marekani katika eneo ni kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sayyid Hassan Nasrallah amelitazama suala hili kwa mtazamo mwingine na anaamini kuwa,  kuimarishwa nafasi ya harakati za muqawama katika eneo la Asia Magharibi ni jambo ambalo limepelekea kudhoofika na kuingiwa na kiwewe utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi tegemezi za Kiarabu. Ni kwa sababu hii ndio Marekani inasisitiza kuwepo wanajeshi wake katika eneo ili kulinda usalama wa utawala wa Israel na tawala za Kiarabu ambazo ni vibaraka wake.

Wapiganaji wa Harakati ya Hashd al Shaabi ya Iraq

Katika mahojiano yake Sayyid Hassan Nasrallah pia amegusia suala la stratijia ya Israel nchini Syria. Katika kipindi cha miaka 9 iliyopita, Israel imejaribu kujiweka mbali na matukio ya Syria kwa matumaini kuwa nchi za Kiarabu kwa msaada wa makundi ya kigaidi zitaweza kuiangusha serikali halali ya Syria.

Lakini kinyume na matarajio hayo ya Wazayuni, serikali ya Syria haikuangushwa na imeweza kuimarika kutokana na msaada wa makundi ya muqawama na uungaji mkono wa Russia na Iran. Aidha makundi ya kigaidi ambayo yamekuwa yakipata himaya ya madola makubwa ya kigeni sasa yanakaribia kusambaratishwa kikamilifu.

Stratijia ya Israel katika hali hiyo imekuwa ni kutekekeleza mashambulizi ya mara kwa mara nchni Syria kwa lengo la kuidhuru Iran na Hizbullah. Kuhusiana na hili, Sayyid Hassan Nasrallah amesema pamoja na kuwepo mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria, lakini utawala wa Kizayuni unachukua tahadhari usiwaue wapiganaji wa Hizbullah kwani unaogopa jibu kali la Hizbullah na inafahmu vyema kwamba vita vyovyote vya pande mbili vitapelekea kuangamia kwake.