Utawala unaotenda jinai wa Israel watumia mabavu dhidi ya waandamanaji
Waisraeli ambao wamekuwa wakiandamana kupinga baraza la mawaziri la waziri mkuu Benjamin Netanyahu wamekabiliwa na utumiaji mabavu wa wanajeshi wa Israel.
Katika wiki za hivi karibuni, ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) zimekuwa zikishuhudia maandamano makubwa dhidi ya baraza la mawaziri la waziri mkuu Benjamin Netanyahu. Maandamano hayo yametokana na utendaji mbovu wa Netanyahu katika kukabiliana na janga la corona katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu sambamba na kuongezeka matatizo ya kiuchumi. Mbali na hayo, Waisraeli wanaamini kuwa baraza la mawaziri la Netanyahu pia ni kitovu cha ufisadi wa kifedha na kimadili. Kwa msingi huo mchanganyiko wa mgogoro wa kiafya na kiuchumi pamoja na ufisadi umepelekea kuibuka wimbi kubwa la maandamano dhidi ya Netanyahu na baraza lake la mawaziri. Waandamanaji Waisraeli wamekusanyika nje ya nyumba ya Netanyahu ambapo mbali na kubainisha kutoridhishwa na utendaji wake, wametaka ajiuzulu kama waziri mkuu. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uluofanywa na Kanali ya 13 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni, asilimia 58 ya Waisraeli hawaridhishwi na utendajikazi wa Netanyahu.
Kuenea wigo wa maandamano na kuongezeka idadi ya waandamanaji kumepelekea wanajeshi wa Israel kukithirisha utumiaji mabavu na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji. Wanajeshi na polisi wa utawala wa Kizayuni wametumia nguvu ziada katika kuwakandamiza na kuwatawanya waandamanaji waliokusanyika mbele ya nyumba ya Netanyahu katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu. Katika makabiliano hayo ya Alkhamisi usiku Wazayuni 55 waliokuwa wakiandamana walikamatwa. Utumiaji mabavu dhidi ya waandamanaji Waisraeli unajiri wakati ambao, gazeti la Kizayuni la Haaretz limeandika kuwa, maandamano hayo yalikuwa ya amani na kwamba hatua ya wanajeshi kuwahujumu waandamanaji ndio iliyokuwa chanzo cha ghasia na machafuko.

Si tu kuwa polisi wamewakamata waandamanaji kwa mabavu bali pia wamewatesa Wazayuni waliokamatwa. Polisi wa utawala haramu wa Israel wanatumia mbinu iliyotumiwa na polisi ya Marekani dhidi ya George Floyd, raia mwenye asili ya Afrika aliyeuawa kinyama Mei 25 katika jimbo la Minnesota. Floyd alibinywa shingo na polisi mzungu kwa muda wa dakika tisa hadi alipokata roho. Kinachotofautiana kati ya ukatili wa polisi wa Marekani na Israel ni kuwa huko Marekani kitendo hicho kilitokana na wazungu kuwabagua watu wenye asili ya Afrika lakini huko Israeli kinachoshuhudiwa ni malumbano ya Wazayuni kwa Wazayuni. Kadhia hii inaonyesha kuwa, ukatili na utumiaji mabavu ni dhati na utambulisho usioteganika na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakalia Quds Tukufu kwa mabavu. Wapalestina wamekuwa waathirika wa muda mrefu wa ukatili wa wanajeshi wa utawala haramu wa Israel. Huu ni utawala ambao sasa umewageukia Wazayuni ambao wanakosoa utendaji kazi wake.
Muamala usio wa kibinaadamu wa vikosi vya usalama vya utawala wa Kizayuni katika kukabiliana na waandamanaji, hasa kumbinya shingo mwandamanaji mmoja, ni jambo ambalo limeibua hasira miongoni mwa Wazayuni na hivyo kushadidisha maandamano na waandamanaji.

Moshe Ya'alon waziri wa zamani wa vita wa utawala haramu wa Israel ni kati ya wanasiasa wa ngazi za juu ambao wanampinga vikali Netanyahu kutokana na mabavu yanayotumiwa na vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji.
Hivi sasa Netanyahu anakabiliwa na mgogoro mkubwa. Mbali na kuwa maandamano yameshadidi, waandamanaji pia wanamtaka ajiuzulu na hilo limekithirisha hitilafu katika muungano wake tawala na Benny Gantz kinara wa chama cha Buluu na Nyeupe. Hitilafu hizo zimepelekea kuongezeka uwezekano wa kusambaratika baraza la mawaziri la Netanyahu na hilo linaonyesha kuwa, kuunda baraza la mawaziri la mseto si tu kuwa hakujasaidia kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa Israel bali kumepelekea kuongezeka migogoro katika utawala huo bandia.