Sep 11, 2020 07:36 UTC
  • Kupunguzwa askari wa Marekani nchini Iraq, hatua ya hiari au isiyo na budi?

Rais Donald Trump wa Marekani aliahidi na kusisitiza wakati wa kampeni zake za uchaguzi kwamba, endapo atachaguliwa kuwa Rais basi atayaondoa majeshi ya nchi hiyo yaliyopo katika eneo la Asia Magharibi.

Licha ya ahadi hiyo, lakini katika miaka ya hivi karibuni, kivitendo Marekani imeongeza idadi ya wanajeshi wake huko Iraq. Hivi sasa baada ya kushadidi upinzani ndani ya Iraq dhidi ya uwepo wa majeshi ya Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu, Pentagon imelazimika kutangaza kuwa, itaondoa kundi la askari wake huko Iraq na kuwarejesha nyumbani.

Jenerali Kenneth Mckenzie, Mkuu wa komandi ya kigaidi ya askari wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) alitangaza katika safari yake huko Iraq kwamba, katika mwezi huu wa Septemba Pentagon itapunguza askari wake hadi kufikia 3000 katika nchi hiyo kutoka 5600. Hatua hiyo ya awali ni ya kipekee tangu mwaka 2016 na katika fremu ya uratibu na serikali ya Iraq pamoja na washirika wa Marekani katika kile kinachojulikana kama vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh.

Jenerali Mckenzie alidai kuwa, hatua hiyo inachukuliwa kutokana na hatua kubwa iliyopigwa na jeshi la Iraq katika kuimarika na kupata nguvu. Hiii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita jenerali huyo alitangaza kuwa, kuna uwezekano majeshi ya Marekani yakabakia kwa muda mrefu nchini Iraq.

Jenerali Kenneth Mckenzie, Mkuu wa komandi ya kigaidi ya askari wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM)

Aidha katika mazungumzo yake hivi karibuni na Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq, Rais Donald Trump alitangaza kuwa, wanajeshi wa nchi yake wataondoka Iraq katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Aidha kabla ya hapo pia, Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba, hatua ya kuwaondoa wanajeshi wa Marekani huko Iraq itatekelezwa kivitendo haraka.

Jenerali Kenneth Mckenzie, Mkuu wa komandi ya kigaidi ya askari wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) anadai kwamba, hatua hiyo ya Washington inatokana na kupata nguvu vikosi vya Iraq, na kukwepa kuashiria ukweli huu kwamba, hatua hiyo imetokana na mashinikizo na kuongezeka upinzani wa Wairaqi dhidi ya uwepo wa majeshi ya Marekani katika nchi yao sambamba na kuongezeka mashambulio dhidi ya askari hao vamizi. Hashim al-Kindi, Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha al-Hadaf cha Iraq sambamba na kusisitiza kwamba, Wamarekani hawataki kuondoka Iraq amesema kuwa, kuondoka Marekani hivi karibu katika baadhi ya kambi za kijeshi huko Iraq, kiuhakika si kitu kingine ghairi ya kutaka kujipanga tena upya.

Baada ya kuuawa kikatili aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH Brigedia Jenerali Qassim Suleimani na Abu Mahd al-Mohandes aliyekuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea Wananchi la Hashd al-Sha'abi la Iraq pamoja na watu waliokuwa wameandamana nao Januari 3 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Baghdad jinai iliyofanywa na Marekani, Bunge la Iraq baada ya siku mbili yaani Januari 5 lilipiga kura na kupasisha takwa la kuondoka nchini humo vikosi vya muungano dhidi ya Daesh vyakiwemo majeshi ya Marekani.

Wanajeshi wa Marekani Iraq

 

Pamoja na hayo, Marekani iliendelea kung'ang'ania kubakia Ireq kinyume cha sheria. Jambo ambalo Marekani inajaribu kulipuuza waziwazi ni kwamba, baada ya kupasishwa muswada katika Bunge la Iraq unaotaka kuondoka nchini humo muungano unaojulikana kama dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh vikiwemo vikosi vya Marekani, kuendelea kuweko majeshi ya Washington huko Iraq ni kinyume cha sheria na maana yake ni kudharua wazi mamlaka ya kitaifa ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Sambamba na hilo, hivi sasa majeshi ya Marekani huko Iraq yanahesabiwa kuwa ni vikosi vamizi. Pentagon ikiipuuza kikamilifu serikali kuu ya Iraq, mara kadhaa imechukua hatua ya kushambulia vituo vya Harakati ya Hashd al-Shaabi kwa kisingizio cha kujibu mashambulio ya roketi dhidi ya kambi zake za kijeshi, bila hata kuitaarifu serikali ya Baghdad kuhusiana na mipango yake hiyo ya mashambulio. Ukweli wa mambo ni kuwa, utendaji huu wa Marekani nchini Iraq ni utendaji wa utawala vamizi ambapo Washington imeendelea kukiuka waziwazi mamlaka ya kujitawala Iraq.

Hatua hizo zimekabiliwa na radiamali hasi ya Wairaqi ambapo katika miezi ya hivi karibuni, mashambulio dhidi ya vikosi vya Marekani huko Iraq yamechukua mkondo wa kuongezeka. Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, mashambulio dhidi ya misafara ya majeshi ya Marekani nchini Iraq yameongezeka mno. Katika kipindi hicho, kwa akali kumeripotiwa matukio 20 ya mashambulio ya mabomu ya kutegwa barabarani dhidi ya misafara ya askari wa Marekani na muungano wa kimataifa eti wa kupambana na ugaidi.

Raios Donal Trump wa Marekani

 

Jambo jingine linalodhihirika wazi katika uwanja huu ni kuwa, suala la kuondoka askari wa Marekani kutoka Iraq linafanyika sasa katika fremu ya kutekeleza ahadi za uchaguzi alizotoa Trump katika kampeni za uchaguzi mwaka 2016 ambapo aliahidi kuondoa majeshi ya nchi hiyo huko Iraq na Afghanistan. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, hatua ya sasa ya serikali ya Trump hasa kwa kuzingatia kukaribia uchaguzi wa Marekani hapo Novemba mwaka huu inalenga kujipigia propaganda kwa wapiga kura.

Pamoja na hayo hatupaswi kusahau kwamba, Trump ameshindwa kabisa kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi kwamba, atahitimisha  vita vilivyobakia vya Marekani duniani kote. Hivi sasa walimwengu wanashuhudia Marekani ikiendelea na sera na hatua zake zile zile za kupenda vita katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Tags