Yemen: Marekani ni mama wa ugaidi na mtengenezaji wa migogoro
Mkurugenzi wa Idara ya Baraza Kuu ya Siasa ya Yemen amesema kuwa Marekani ndio mama wa ugaidi na muanzishaji wa migogoro inayolisumbua taifa la Yemen.
Ahmad Hamid amesema katika uzinduzi rasmi wa kampeni ya wananchi iliyopewa anwani ya: "Jinai za Marekani Mvamizi dhidi ya Yemen", iliyofanyika jana mjini Sanaa kwamba, Marekani ni adui halisi wa taifa la Yemen na watawala wa ukoo wa Aal Saud wa Saudia wanapigana vita kwa niaba ya serikali ya Washington.
Ahmad Hamid ameongeza kuwa, lengo la kampeni hiyo ni kufichua jinai na uhalifu unaofanywa na Marekani kwa watu wa Yemen.
Mkurugenzi wa Idara ya Baraza Kuu la Siasa nchini Yemen amesema kuwa, Marekani imefanya uhalifu na jinai kubwa na nyingi na kuongea kuwa: Vyombo vya habari vina jukumu la kunyanyua juu uelewa wa wananchi kuhusu uhalifu huo wa Washington.
Marekani ni mfadhili na muungaji mkono mkuu wa vita vya Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen.
Hivi karibuni harakati ya Ansarullah ya Yemen ilifichua nyaraka za siri za ushirikiano wa Marekani na muungano vamizi wa Saudia katika mauaji ya maelfu ya raia wasio na hatia wa Yemen.