Maseneta wa Marekani wapanga kuzuia mauzo ya silaha kwa Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i64716-maseneta_wa_marekani_wapanga_kuzuia_mauzo_ya_silaha_kwa_imarati
Maseneta watatu wa Marekani wamesema wanataka kuwasilisha miswada ya kuizuia serikali ya hivi sasa ya Donald Trump kuiuzia silaha Imarati.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2020 03:45 UTC
  • Maseneta wa Marekani wapanga kuzuia mauzo ya silaha kwa Imarati

Maseneta watatu wa Marekani wamesema wanataka kuwasilisha miswada ya kuizuia serikali ya hivi sasa ya Donald Trump kuiuzia silaha Imarati.

Maseneta watatu hao wa chama tawala cha Republican, ambao ni Bob Menendez, Chris Murphy na Rand Paul walisisitiza jana Jumatano kwamba wanapanga kuwasilisha miswada minne ambayo itazuia nchi hiyo ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuuziwa ndege zisizo na rubani, ndege za kivita aina ya F35 na makombora ya anga kwa anga yenye thamani ya dola bilioni 23.

Kwa mujibu wa maseneta hao, serikali ya Trump ina mpango wa kuiuzia Imarati silaha za Marekani zikiwemo ndege za kivita za kisasa kabisa, makombora zaidi ya 14,000 na zana nyingine za kijeshi.

Vita vya kichokozi dhidi ya Yemen

Awali Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alikuwa ametangaza kuwa serikali ya Washington tayari imepasisha mpango wa kuiuzia nchi hiyo ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi silaha zenye thamani ya dola bilioni 23.

Upinzani wa maseneta hao wa Marekani unabainishwa katika hali ambayo tayari serikali ya Trump ni mmoja wa wadhamini wakubwa wa silaha kwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen.

Imarati ni moja ya nchi zilizo kwenye muungano huo wa vita dhidi ya Yemen, vita ambavyo hadi sasa vimepelekea kuuawa na kujeruhiwa  makumi ya maelfu ya watu wa nchi hiyo masikini ya Kiarabu.