Marekani inaunda 'ISIS 2' katika nchi za Syria na Iraq
Ushahidi mpya umefichua kuwa, vyombo vya usalama vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel vipo mbioni kuzalisha kizazi kipya cha genge la kigaidi katika eneo hili la Asia Magharibi.
Shirika la habari la IRNA limenukuu duru za kuaminika zikisema kuwa, wanasaikolojia wa usalama wa Marekani kwa kushirikiana na vikosi vya kiintelijensia vya utawala haramu wa Israel wanasajili na kuwapa mafunzo ya kijeshi watu wa familia za wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) walioko katika kambi ya wakimbizi ya al-Hol katika mkoa wa al-Hasakah kaskazini mashariki mwa Syria.
Inaarifiwa kuwa, familia hizo mbali ya kupewa mahitaji ya msingi ya kila siku na Marekani, Uingereaza na Israel kambini hapo, lakini zinapewa pia vitabu vya kitakfiri kama kile kiitwacho 'Taifa la Ibrahim' kilichoandikwa na al-Maqdisi. Kitabu hicho cha 'The Nation of Ibrahim' kimetumika pia katika kambi ya Bucca katika mji wa Ummul Qasr katika mkoa wa Basra kusini mwa Iraq kuunda kizazi kipya cha ISIS (ISIL 2).
Habari zaidi zinasema kuwa, Marekani na Wazayuni wanafanya juu chini kuwarubini wanawake na vijana kujiunga na kizazi hicho kipya cha ISIS katika nchi za Iraq na Syria.
Aprili mwaka huu, chanzo kimoja cha usalama nchini Iraq kilisema kuwa, kwa mujibu wa taarifa za kiintelejensia zilizopatikana, Abu Ibrahim al-Hashimi al-Qurashi, kiongozi mpya wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) amepenya nchini humo kwa msaada wa askari magaidi wa Marekani.
Hii ni katika hali ambayo, taifa la Iraq linaadhimisha kumbukumbu ya kutimia mwaka wa tatu tangu lipate ushindi dhidi ya kundi hilo la kigaidi nchini humo, ingawaje operesheni za kuwasaka mabaki ya mamluki wa kundi hilo la ukufurishaji zingali zinaendelea.