Jan 06, 2021 02:45 UTC
  • Wanajeshi wa Marekani nchini Iraq; mwaka mmoja baada ya kupasishwa mpango wa Bunge

Jumanne ya jana tarehe 5 Januari ilisadifiana na kutimia mwaka mmoja tangu Bunge la Iraq lilipopasisha mpango wa kufukuzwa nchini humo askari wa Marekani.

Mpango huo ulikuwa ni radiamali ya jinai ya serikali ya kigaidi ya Marekani ya kumuua Luteni Jenerali Qassim Suleimani, Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, Abu Mahdi al-Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Harakati ya al-Hashd al-Shaabi na wanamapambano wenzao wanane, katika shambulio la anga lililofanywa karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq. Umepita mwaka mmoja tangu mpango huo ulipopasishwa na Bunge la Iraq. Licha ya wananchi kuunga mkono hatua hiyo, suala la kuondoka askari wa Marekani nchini Iraq limeendelea kuwa sehemu ya mvutano baina ya serikali na mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo.

Serikali ya Iraq imefanya duru kadhaa za mazungumzo na serikali ya Washington kuhusiana na kadhia ya kuondoka nchini humo askari wa Marekani. Serikali ya Iraq chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Mustafa al-Kadhimi haijachukua msimamo wa wazi na wa kueleweka kuhusiana na kadhia hii. Hata hivyo Rais Donald Trump alitangaza Agosti mwaka jana wakati al-Kadhimi alipofanya safari mjini Washington kwamba,  wanajeshi wa nchi yake huko Iraq wataondoka katika nchi hiyo  ya Kiarabu kwa awamu katika kipindi cha miaka mitatu.

Maandamano makubwa ya Wairaqi dhidi ya uwepo wa askari wa Marekani katika nchi yao

 

Msimamo huo wa Trump ulikabiliwa na malalamiko makubwa ya makundi mbalimbali ya Iraq. Katika upande wa kivitendo, Novemba mwaka jana askari 500 wa Marekani walianza kuondoka nchini Iraq. Swali muhimu linaloulizwa na weledi wa mambo ni kuwa, kwa nini uamuzi uliopasishwa na Bunge la Iraq unaotaka kuondoka askari wa Marekani nchini humo haujatekelezwa kivitendo?

Inaonekana kuwa, sababu kuu inayokwamisha jambo hilo ni kutokuweko kauli na msimamo mmoja baina ya makundi na mirengo ya kisiasa nchini Iraq. Licha ya kuwa Bunge la Iraq lilipasisha mpango wa kuondoka askari wa Marekani nchini humo, lakini aghalabu ya makundi na mirengo ya Kisuni na Kikurdi na baadhi ya miungano ya Kishia inapinga mpango huo. Hata kikao cha Bunge cha Januri 5 mwaka jana cha kupigia kura muswada huo kilisusiwa na makundi hayo.  Ukweli wa mambo ni kuwa, baadhi ya makundi ya kisiasa ya Iraq yanaaamini kuwa, kuondoka nchini humo askari wa Marekani kunakinzana na maslahi na usalama wao, na ndio maana hayaafiki kutekelezwa uamuzi huo wa Bunge.

Kwa muktadha huo basi, inaoenekana ndani ya Bunge la Iraq kuna mgawanyiko mkubwa baina ya wapinzani na wale wanaoafiki kuondoka askari wa Marekani nchini humo. Katika majimui ya Wabunge wote 329 ni Wabunge 168 tu ndio ambao Januari 5 mwaka jana waliupigia kura ya ndio mpango unaotaka kuondoka nchini humo askari wa kigaidi wa Marekani. Kwa maana kwamba, ni wabunge watatu zaidi tu baada ya nusu ya idadi ya Wabunge wote wa nchi hiyo.

Rais Donald Trump alipowatembea askari wa Marekani nchini Iraq

 

Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr baada ya zoezi hilo la upigaji kura aliwahutubu Wabunge kwa kuandika: Mimi ninaona kura za kupasishwa muswada huu zilizopigwa ni jibu dhaifu na lisilotosha kwa hatua ya ukiukaji mamlaka ya kujitawala Iraq unaofanywa na Marekani pamoja na hatua za Washington za kushadidisha mizozo na mivutano katika eneo la Asia Magharibi.

Sababu nyingine muhimu ni kutokuweko azma na irada ya kweli ya serikali ya Iraq ya kufuatilia mpango uliopasishwa na Bunge la nchi hiyo unaotaka kutimuliwa nchini humo askari vamizi wa Marekani. Mustafa al-Kadhimi alichukua wadhifa wa Uwaziri Mkuu baada ya kuungwa mkono na kupigiwa kura ya kuwa na imani naye na makundi yote matatu nchini humo ya Mashia, Masuni na Wakurdi. Baadhi ya makundi ya Iraq ni tegemezi na yenye mfungamno wa moja kwa moja na Marekani na yamekuwa yakipata himaya na uungaji mkono kutoka kwa Washington.

Kwa upande mwingine, Iraq ni nchi ambayo ipo chini ya uvamizi wa Marekani ambayo ilikuwa na kambi na vituo 14 vya kijeshi katika nchi hiyo. Ingawa baada ya kupasishwa mpango wa Bunge la Iraq Januari 5 mwaka jana, vituo 4 kati ya hivyo vimefungwa. Kwa msingi huo basi inawezekana kusema kuwa, si tu kwamba, serikali ya Baghdad haina mamlaka ya lazima na ya kutosha ya kuwafukuza askari wa Marekani nchini humo, bali hata Waziri Mkuu wa Iraq mwenyewe Mustafa al-Kadhimi anaona kuwa anahitajia himaya ya Washington ili aendelee kubakia uongozini.

Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq

 

Sababu nyingine muhimu inayoashiriwa na weledi wa mambo ni kuwa, Iraq na Marekani zilitiliana saini hati ya makubaliano ya usalama mwaka 2008 na 2014. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Marekani iliasisi na kujenga vituo vya kijeshi nchini Iraq na kutumia gharama kubwa kwa ajili ya shughuli hiyo. Marekani inataka ilipwe gharama za ujenzi wa vituo hivyo ndipo iondoe askari wake katika nchi hiyo. Hata hivyo kwa sasa serikali ya Baghdad haiko katika mazingira mazuri kwa upande wa kifedha hata iweze kufidia gharama hizo zinazotakiwa na serikali ya Washington.

Majimui ya mazingira haya ndiyo yaliyopelekea kutochukuliwa hatua ya maana ya kuwatimua askari wa Marekani nchini Iraq licha ya kupita mwaka mmoja tangu Bunge la nchi hiyo lipasishe mpango huo. Hata hivyo ukweli wa mambo ni kuwa, mazingira ya leo wanayokabiliwa nayo wanajeshi wa Marekani huko Iraq yanatofautiana kikamilifu na hali ya mambo ilivyokuwa kabla ya tarehe 5 Januari mwaka uliopita wa 2020 siku Bunge la nchi hiyo lilipopasisha uamuzi wa kutimuliwa wanajeshi hao kutoka Iraq.

Hii leo askari wa Marekani nchini Iraq hawana usalama na wamekuwa wakiishi katika mazingira ya hofu na wahaka. Hali hiyo imeifanya Marekani ilazimike kufunga baadhi ya vituo vyake vidogo vya kijeshi na kuwapeleka askari hao katika vituo vikubwa. Kwa mintarafu hiyo inaonekana kuwa, licha ya sababu tulizotangulia kuzitaja, mpango wa kuondoka askari wa utawala wa kigaidi wa Marekani nchini Iraq utachukua muda, lakini lisilo na shaka ni kuwa, mwisho wa siku askari hao watalazimika kufungasha virago na kuondoka katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Tags