Netanyahu kizimbani kujibu mashitaka ya ufisadi, maandamano yashtadi
(last modified Mon, 08 Feb 2021 12:04:56 GMT )
Feb 08, 2021 12:04 UTC
  • Netanyahu kizimbani kujibu mashitaka ya ufisadi, maandamano yashtadi

Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu amepandishwa kizimbani, kujibu mashitaka ya ufisadi yanayomkabili, huku faili lake likifunguliwa upya wiki chache kabla ya kufanyika uchaguzi wa Bunge.

Netanyahu amefika katika Mahakama ya Wilaya mjini Quds (Jerusalem) leo Jumatatu chini ya ulinzi mkali, huku maandamano dhidi yake yakichachamaa.

Hii ni mara ya pili kwa Netanyahu kufika mahakamani yeye binafsi kujibu mashitaka ya ufisadi wa kifedha na kupokea rushwa yanayomuandama kwa miaka kadhaa sasa.

Pamoja na mashitaka mengine, Netanyahu na mke wake Sara wameshtakiwa kwa kupokea hongo na zawadi zenye thamani kubwa. Waandamanaji huku wakiwa na mabango yenye jumbe zinazosema "Netanyahu, Waziri wa Ufisadi" na "Jiuzulu" wamemtaka mwanasiasa huyo aachie ngazi mara moja. 

Maandamano ya Waisraeli dhidi ya Netanyahu

Waisraeli wamekuwa wakishiriki maandamano makubwa yanayofanyika kila wiki mjini Tel Aviv dhidi ya Netanyahu, licha ya kukabiliwa kwa mkono wa chuma na maafisa usalama na bila kujali msambao wa virusi vya corona.

Wakazi wa ardhi hizo za Palestina zinazokaliwa kwa mababu wamekuwa wakifanya maandamano hayo tokea Mei mwaka jana kwa ajili ya kumlazimisha Netanyahu ajiuzulu na kutoshiriki katika serikali ijayo.