Russia: Saudia ikiingia kijeshi Syria ni sawa na tangazo la vita
Naibu Spika wa bunge la Russia ameitahadharisha Saudi Arabia kuhusu kupeleka wanajeshi wake nchini Syria na kusema kuwa, hatua kama hiyo itachukuliwa kama tangazo la vita endapo haitapata ridhaa ya serikali ya Damascus.
Pavel Krasheninnikov amesema sheria za kimataifa zinazuia nchi yoyote kupeleka majeshi katika nchi nyingine bila ya ridhaa ya serikali husika. Pavel amesema hayo siku moja baada ya Saudi Arabia kutangaza kuwa iko tayari kupeleka wanajeshi wa nchi kavu huko Syria eti kupambana na kundi la kigaidi la Daesh.
Kauli ya Saudi Arabia ya kupeleka wanajeshi katika ardhi ya Syria imetolewa baada ya magaidi wa Daesh kupata pigo kubwa kufuatia kuondolewa kwao na jeshi la Syria katika maeneo muhimu ya mkoa wa Aleppo na kukatwa njia yao ya kusafirishia bidhaa kutoka Uturuki.
Saudia ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa magaidi wa Daesh na makundi mengine ya kigaidi ndani ya Syria inataka kutuma majeshi yake ili badala ya kupambana na magaidi iweze kushambulia vikosi vya serikali na kurudisha mlingano katika vita vya Syria ambavyo kwa sasa vinaonekana kudhibitiwa na jeshi la serikali ya Damascus.