Syria yakanusha madai ya kufanya mazungumzo ya siri na Israel
Syria imekanusha vikali ripoti zinazodai kuwa maafisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo ya Kiarabu wanafanya mazungumzo ya siri na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Shirika rasmi la habari la Syria (SANA) limenukuu vyanzo vya habari ndani ya serikali ya Syria vikisema kuwa, madai hayo yaliyoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu eti mazungumzo ya siri na Wazayuni hayana ukweli wowote, bali ni ya uongo na ya kipropaganda.
Taarifa ya vyanzo hivyo vya habari imeeleza bayana kuwa: Serikali ya Damascus haijawahi kufuata mfumo huo wa mazungumzo ya siri na kwamba msimamo wa nchi hiyo ya Kiarabu kwa utawala pandikizi wa Israel uko wazi na unajulikana.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, madai kuwa kuna mazungumzo hayo eti ya siri baina ya Tel Aviv na Damascus kwa lengo la pande mbili hizo kufikia makubaliano ya amani ni uvumi na porojo za kisiasa na za vyombo vya habari vya Wamagharibi.
Hivi karibuni pia, baadhi ya vyombo vya habari vya Kizayuni vilieneza uvumi kwamba, baada ya Imarati, Bahrain, Sudan na Morocco, Iraq nayo imekubali kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Baghdad ilikanusha vikali madai hayo.
Hadi hivi sasa nchi hizo nne za Kiarabu zilizojidhalilisha kwa Wazayuni zinaendelea kulaaniwa katika ulimwengu mzima wa Kiislamu na Kiarabu.