Jeshi la Syria lazima tena shambulio la makombora la Israel
Kwa mara nyingine tena, Jeshi la anga la Syria limekabiliana na shambulizi la makombora la utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Rif Dimashq, viungani mwa mji mkuu Damascus usiku wa kuamkia leo.
Duru za kijeshi zimetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni umeshambulia kwa makombora kadhaa eneo hilo usiku wa jana, lakini ngao ya makombora ya jeshi la anga la Syria imefanikiwa kusambaratisha aghalabu ya makombora hayo kabla ya kufika yaliyokusudiwa.
Aidha shirika rasmi la habari la Syria SANA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, hujuma hiyo ya anga ya utawala vamizi wa Israel imefanyika karibu na Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Damascus.
Habari zaidi zinasema kuwa, jeshi katili la Israel limetekeleza uchokozi huo mpya kutoka Miinuko ya Golan ya Syria inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo khabithi.
Mara kwa mara utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Syria hasa dhidi ya miundombinu na maeneo ya wanajeshi wa nchi hiyo ya Kiarabu.
Pamoja na mambo mengine, utawala wa Kizayuni unafanya mashambulizi hayo kwa lengo la kuwaunga mkono magaidi na kuwatia moyo kila wanapopata kipigo kutoka kwa jeshi la Syria.