Naim Qassim: Kushikamana Waislamu kumesambaratisha njama za US-Israel
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuungana na kushikamana Waislamu pasina kujali tofauti zao za kimitazamo na kiitikadi kumesambaratisha njama za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel za kuyagawanya vipande vipande mataifa ya Kiislamu.
Sheikh Naim Qassim amesema hayo katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu ya Kiislamu, Hamid Shahriari jana usiku na kuongeza kuwa, njama za maadui Wamarekani na Wazayuni za kuwagawanya Waislamu kwa misingi ya kimadhehebu zimegonga mwamba.
Amebainisha kuwa, kitendo cha kuyakuribusha pamoja madhehebu za Kiislamu kimetoa pigo kubwa na athirifu kwa maadui waliotaka kuyagawanya mataifa ya Kiislamu kwa kutumia magenge ya kitafkiri, ugaidi na tofauti za kiutamaduni.
Mwanachuoni huyo mashuhuri wa Lebanon ameeleza bayana kuwa, Marekani na utawala haramu wa Israel zilikuwa na azma ya kutumia njama hizo si tu kuibua vita vya kimedhehebu lakini pia vita vya kidini katika eneo la Asia Magharibi.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, harakati hiyo ya muqawama daima ina hamu ya kufanya mazungumzo na makundi tofauti ya nchi hiyo pamoja na kushirikiana nayo; sanjari na kukabiliana na maadui wa taifa hilo la Kiarabu na wa umma wa Kiislamu kwa ujumla.