Ripoti ya kwanza ya "Hiroshima ya Yemen" yasambazwa na Ansarullah
Idara ya masuala ya haki na sheria ya Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen, imesambaza ripoti ya kwanza ya kisheria na ya matukio ya kweli kuhusu jinai za kutisha na za kinyama za Saudi Arabia na Marekani dhidi ya wananchi wa Yemen. Ripoti hiyo imepewa jina la Hiroshima ya Yemen.
Mtandao wa habari wa al Ahd wa nchni Lebanon umetangaza habari hiyo na kumnukuu Abdul Wahab al Mahbashi, mkuu wa idara ya masuala ya haki na sheria ya Ofisi ya Kisiasa ya Ansarullah ya Yemen akisema hayo jana Alkhamisi katika sherehe za uzinduzi wa ripoti ya Hiroshima ya Yemen na kuongeza kuwa, ripoti hiyo imewafedhehesha na kuwatetemesha wavamizi ambao muda wote wamekuwa wakijaribu kukanusha na kuficha jinai zao hizo kubwa za kinyama kwa wananchi wa Yemen.
Amesema, wavamizi wanajaribu kila wawezavyo kuficha jinai kubwa wanazotenda nchini Yemen na wanatumia njia mbalimbali kama vile kusambaza ripoti za uongo ili kuzipotosha fikra za walimwengu, lakini mfululizo wa ripoti za Hiroshima ya Yemen utawafedhehesha wavamizi hao wanaofanya jinai na mauaji ya halaiki na ya kikatili mno huko Yemen.
Katika upande mwingine, Ahmad Abu Hamra, afisa wa kituo cha kukusanya taarifa za kina cha idara hiyo ya Ansarullah amesema, ripoti hii ya kwanza ina kurasa 4133 zinazohusiana na mauaji ya umati yaliyofanywa na wavamizi wa Yemen wakiongozwa na Saudi Arabia na zimetoa ufafanuzi wa kina ikiwa ni pamoja na wakati na maeneo zilipofanywa jinai hizo.
Huku hayo yakiripotiwa, siku chache zilizopita, wizara ya usafiri na uchukuzi ya serikali ya wokovu wa kitaifa ya Yemen ilisema, Wayemen 80,000 wamefairki dunia kwa sababu ya kufungwa kwa muda wa miaka sita uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sana'a.
Kwa mujibu wa ripoti ya pamoja iliyotolewa Jumatatu wiki hii na wizara hiyo pamoja na idara zilizo chini yake, kuzingirwa kila upande Yemen na kufungwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sana'a kwa muda wa miaka sita, kumepelekea kufariki dunia raia 80,000 wa nchi hiyo waliokuwa wakihitaji matibabu ya haraka baada ya kushindikana kuwasafirisha nje ya nchi.