Vita vya Yemen kwa mtazamo wa Sayyid Hassan Nasrullah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i68582-vita_vya_yemen_kwa_mtazamo_wa_sayyid_hassan_nasrullah
Katika sehemu ya hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya Sheikh al-Qadhi Ahmad az-Zain hapo siku ya Jumatano, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliashiria kadhia ya vita vya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2021 06:07 UTC
  • Vita vya Yemen kwa mtazamo wa Sayyid Hassan Nasrullah

Katika sehemu ya hotuba yake kwa mnasaba wa maadhimisho ya Sheikh al-Qadhi Ahmad az-Zain hapo siku ya Jumatano, Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon aliashiria kadhia ya vita vya Yemen.

Vita vya muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen vilianza tareher 26 Machi 2015 na sasa vita hivyo vimeingia katika mwezi wa kwanza wa mwaka wake wa saba. Kuna sababu tofauti zinazotolewa na waungaji mkono na wapinzani wa muungano huo kuhusu chanzo cha vita hivyo. Sayyid Nasrullah ambaye ni miongoni mwa watu mashuhuri wanaopinga vita, amesema kwamba vita vya Yemen vilianza kutokana na mtazamo wa kimadhehebu na kimakundi wa watawala wa Saudi Arabia kuhusu masuala ya Yemen.

Kimsingi Saudi Arabia imeligawa eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) katika makundi mawili ya Shia na Sunni, na kwa mtazamo huo inapinga na kuichukia kila nchi ya Kishia au iliyo na wakazi wengi wa Kishia. Kwa mtazamo wa Wasaudia hakuna tofauti yoyote iliyopo baina ya Bahrain, eneo la mashariki mwa Saudia, Yemen, Nigeria, Iraq au Iran. Utawala wa Saudi Arabia una mtazamo wa chuki na nchi na maeneo yote hayo.

Mwaka 2011, utawala huo ulitumia nguvu na uwezo wake wote kuzima harakati ya mapambano ya watu wa Yemen dhidi ya dikteta Abdalla Swaleh wa nchi hiyo na hatimaye kufuatilia malengo yake nchini humo kupitia uchaguzi wa kimaonyesho tu wa Februari 2012 uliomuweka madarakani Abdurabbuh Mansur Hadi.

Abdurabbuh Mansur Hadi

Baada ya harakati ya watu wa Yemen kuanza tena mwaka 2014 na hatimaye kumfukuza madarakani kibaraka huyo aliyekimbilia Saudia, watawala wa Riyadh kwa mara nyingine walianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen kwa ajili ya kuwazuia Mashia wasiweze kuchukua madaraka ya nchi hiyo. Kuhusu hilo Sayyid Hassan Nasrullah anasema: Mfumo wa Saudi Arabia ulikuwa unataka kutoa muelekeo maalumu kuhusu vita vya Yemen. Kwa msingi huo mwanzoni mwa uvamizi wa Yemen, mufti wa Wasaudia alidai kuwa vita hivyo vilikuwa ni vita baina ya Masuni na Mashia.

Nukta nyingine iliyozungumziwa na Sayyid Nasrullah kuhusu vita vya Yemen ni kuwa Saudi Arabia imetumbukia katika mtego wa Wazayuni na Wamarekani ambao bila shaka wanachochea hisia na migawanyiko ya kimadhehebu katika Asia Magharibi. Chuki dhidi ya Iran ni sehemu ya siasa za maadui hao wakubwa wa Uislamu. Vita dhidi ya Yemen na makabiliono na kundi la Ansarullah ambalo ni kundi lililo na uungaji mkono mkubwa wa watu wa Yemen vile vile ni sehemu ya siasa za chuki zinazoenezwa na Wazayuni na Wamarekani katika eneo hili kwa ushirikiano wa Saudi Arabia.

Kuhusu hilo Sayyid Nasrullah amesema: Vita vya Yemen havina uhusiano wowote na Ushia na Usunni bali vinatekelezwa kwa malengo ya Marekani na njama zake dhidi ya eneo hili. Silaha ya pekee iliyobakia mikononi mwa Wamarekani na Wazayuni ni kuchochea fitina katika eneo. Kabla ya hapo suala hilo lilikuwa limeashiriwa pia na Abdul Malik al-Houthi, Katibu Mkuu wa Ansarullah mwishoni mwa mwaka wa sita wa vita dhidi ya Yemen.

Katika hotuba yake ya siku ya Jumatano, Sayyid Hassan Nasrullah alisema kuwa maadui wa Yemen hivi sasa wanatumia propaganda kubwa ya vyombo vya habari kujaribu kuonyesha kinyume na ukweli wa mambo kwamba, Ansarullah ya Yemen inapinga kuhitimishwa vita ilihali Saudia ndiyo inatumia juhudi na uwezo wake wote kumaliza vita hivyo. Ni wazi kuwa Saudi Arabia imetenda jinai kubwa za kivita dhidi ya taifa la Yemen na hivi sasa iko chini ya mashinikizo makubwa yanayoitaka isimamishe vita hivyo ambapo imelemewa kijeshi na jeshi pamoja na kamati za kujitolea mhanga za wananchi wa Yemen. Ni kwa msingi huo ndipo utawala wa Saudia ukapaparikia pendekezo la kusitisha vita ambalo limechangamkiwa na Marekani na Umoja wa Mataifa.

Sehemu ya jinai za kivita za Saudia nchini Yemen

Pendekezo hilo halina nia yoyote ya kumaliza vita bali ni usitishaji vita wa muda tu ndio unaokusudiwa, jambo ambalo limepingwa vikali na Serikali ya Wokovu ya Yemen ambayo inataka kusimamishwa mara moja mzingiro na vita vya kidhalimu dhidi ya nchi hiyo na sio usitishaji vita. Huo ni ujanja na hadaa kubwa ambayo hata mtoto mdogo wa Yemen hawezi kuikubali.

Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Sayyid Nasrullah ilihusiana na hatima ya vita vya Yemen. Kwa mtazamo wa Katibu mkuu huyo wa Hizbullah ya Lebanon, Wayemen wanaendelea kupata mafanikio makubwa katika medani ya vita na kwamba ni Wasaudia ndio wanaendelea kupata hasara na madhila katika vita hivyo. Kwa msingi huo amewahutubu Wasaudia kwa kuwaambia: Ninaiambia serikali ya Saudia, msiendelee kupoteza bure wakati wenu. Hadaa haitakusaidieni kwa lolote lile. Amueni kumaliza vita na mzingiro (dhidi ya watu wa Yemen).