"Kuiondoa Ansarullah katika orodha ya ugaidi ni hadaa ya Marekani"
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen amesema hatua ya Marekani ya kutangaza eti imeliondoa jina la Ansarullah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi ni hadaa tupu na mchezo mchafu wa kisiasa.
Mohammad Ali al-Houthi amesema hayo na kufafanua kuwa, tangazo hilo la Marekani ni madai hewa yasiyo na maana kwani nchi hiyo maskini ya Kiarabu ingali chini ya mzingiro, ugaidi na uvamizi.
Amebainisha kuwa, licha ya madai hayo ya Marekani, lakini muungano katili wa kijeshi unaoongozwa na Saudia unaendelea kumwaga damu za Wayemen mbali na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen ameeleza bayana kuwa, kauli ya Marekani kuwa inataka kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kibinadamu unaoikabili Yemen haina ukweli wowote, bali inalenga kuzihadaa fikra za waliowengi.
Hivi karibuni, Wizara ya Fedha ya Marekani ilidai kuwa harakati ya Ansarullah ya Yemen imeondolewa katika orodha ya Washington ya makundi ya kigaidi au yanayounga mkono ugaidi, kama njia moja ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kibinadamu unaolikabili taifa hilo la Kiarabu.
Hadi sasa Wayemeni zaidi ya elfu 16 wameshauawa katika vita vya muungano vamizi unaoongozwa na Saudia tokea Machi 2015, huku makumi ya maelfu ya wengine wakijeruhiwa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.